Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro amesema tayari jeshi hilo limemaliza kuufanyia kazi mwili wa kijana Hamza aliesababisha mauaji ya watu wanne wakiwemo askari polisi watatu na mlinzi wa kampuni binafsi karibu na ubalozi wa Ufaransa na Daraja la Salenda Jijini Dar es Salaam.

IGP Sirro ametoa kauli leo Agosti 28, 2021 wakati Jeshi la Polisi likiwaaga Makamishna wake Balozi Valentino Mulowola na Robert Boaz, huku akiwataka ndugu wa kijana huyo Hamza Mohamed wakauchukue mwili huo kwa ajili ya maziko na endapo watashindwa kuuchukua basi mwili huo utazikwa na Halmashauri.

“Tunawakabidhi ndugu zake kwa sababu tayari sisi tumeshaufanyia kazi kama ndugu zake hawajaja kuuchukua waje wauchukue lakini siku zikifika na hawajaja kuuchukua Halmashauri itaenda kuzika”

“Hiyo familia ya Hamza inajisikiaje, fikiria wewe ungekuwa baba yake Hamza, mama yake Hamza, mdogo wake ungejisikiaje kuzaa kwako umetuletea balaa Watanzania, kwahiyo naomba Watanzania wengine wasituzalie watoto kama Hamza,” Amesema IGP Sirro.

Hamza aliuwawa Agosti 25, 2021 kwa kupigwa risasi na polisi dakika chache baada ya kuwauwa askari polisi watatu na mlinzi wa kampuni binafsi karibu na ubalozi wa Ufaransa na daraja la Salenda jijini Dar es Salaam.

Burna Boy azidi kupasua anga
Vituo maalum vya kuchoma chanjo ya Corona vyafunguliwa uwanja wa mkapa, uhuru