Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya leo Agosti 28, 2021 imeratibu zoezi la hiari la siku mbili kwa timu za Taifa za michezo na wadau wote wa michezo upatiwa chanjo ya Uviko-19 jijini Dar es Salaam ili kujikinga na ugonjwa huo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema makundi hayo yamependekezwa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia kutokana na mazingira ya kazi zao.

“Ninapenda tena leo kuendelea kusisitiza na kuhamasisha wanahabari, wanautamaduni, wasanii na wanamichezo wenzangu kuendelea kupata huduma ya chanjo. Sekta zetu zinahudumia wananchi na hivyo kulazimika kukutana na makundi ya watu mara kwa mara. Kutokana na hivyo tuna hatari kubwa ya kuambukizwa, ama sisi wenyenyewe au kuambukiza wananchi ambao ndio wadau wetu wakubwa tunaowapa huduma. Kwa vyovyote vile ni lazima tujikinge lakini pia tuwakinge wadau wetu,” Amesema Waziri Bashungwa.

Amesema kuwa ili kufanikisha zoezi hilo vimefunguliwa vituo maalum ndani ya uwanja wa Mkapa na Uhuru vitakavyokuwa vikitoa huduma ya chanjo hiyo kuanzia saa 3 asubuhi kwa siku zote mbili  ili kutoa fursa kwa wadau wote kupata huduma hiyo.

Katika hatua nyingine ameupongeza uongozi wa Klabu ya Yanga kwa kutumia wiki ya wananchi kuhamasisha watu kupata chanjo na kulifanya zoezi hilo la uchanjaji kuwa miongoni mwa shughuli zao muhimu watakazo zifanya siku hiyo huku akitoa wito kwa vilabu vingine vya soka nchini kuhamasika na kuwapatia chanjo wachezaji na watumishi wao.

Naye Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuph Singo Omary amemhakikishia  Waziri kuwa maandalizi yote ya zoezi la chanjo yamekamilika na tayari wadau mbalimbali wa michezo wamepongeza hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kuwapa kipaombele wadau ili wajikinge.

Jeshi la Polisi lamaliza uchunguzi mwili wa Hamza
MAGORI: Yale ndio maisha ya Mo Dewji, hawezi kubadilika