Mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona, bado wanaendelea kuumiza vichwa kuhusu mbadala wa Dani Alves ambaye aliamua kutimkia nchini Italia (Juventus FC) mwishoni mwa msimu uliopita.

Taarifa za mipango ya kuziba mwanya ulioachwa na beki huyo kutoka nchini Brazil, jana zilivuja kwa kumuhusisha beki wa kulia wa Stoke City ya nchini England Glenn Johnson, ambaye anapambanishwa na Darijo Srna (Shakhtar Donetsk), Stephan Lichtsteiner (Juventus), Pablo Zabaleta (Manchester City) pamoja na Branislav Ivanovic (Chelsea).

Mapema hii leo jina la beki wa kulia wa Liverpool Nathaniel Clyne nalo limetajwa katika mchakato huo ambao bado unaendelea kufanyiwa kazi na benchi la ufundi la FC Barcelona linaloongozwa na Luis Enrique.

Gazeti la The Sun limeandika kuwa, beki huyo mwenye umri wa miaka 25 huenda akang’olewa Liverpool kwa kiasi cha Pauni milioni 20 itakapofika mwezi januari mwaka 2017.

Kwa sasa hivi FC Barcelona wamekua wanamtumia Sergi Roberto ambaye anasaidiana na Aleix Vidal katika nafasi ya ulinzi wa kulia lakini wameonyesha wanashindwa kukabiliana na changamoto kutoka kwa wapinzani.

Clyne ambaye tayari ameshaitumikia timu ya taifa ya England mara 13, amekua muhimili mkubwa katika kikosi cha Jürgen Klopp na tangu alipojiunga na Liverpool mwaka 2012 ameshacheza michezo 64.

Clyne alijiunga na Liverpool akitokea Southampton ambao walimsajili mwaka 2008 akitokea Crystal Palace.

Ligi Daraja La Kwanza Tanzania Bara Kuunguruma Tena
Ligi Ya Taifa Ya Wanawake Kuzinduliwa Rasmi Mjini Dodoma