Klabu ya VfL Wolfsburg imemtangaza mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden Freddie Ljungberg, kuwa kocha msaidizi, baada ya kulifumua benchi la ufundi mwishoni mwa juma lililopita.

Andries Jonker alitangazwa kuwa kocha wa kikosi cha kwanza kufuatia  Valerien Ismael kutimuliwa klabuni hapo, baada ya kukabiliwa na matokeo mabaya.

Hata hivyo jina la Ljungberg lilipendekezwa na Andries Jonker kabla ya kufikishwa kwa viongozi wa klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya nchini Ujerumani.

Baada ya kutangazwa jina la mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuitumikia Arsenal na West Ham Utd, Jonker alifichua siri ya kupendekeza jina la Ljungberg mbele ya waandishi wa habari.

“Nimempendekeza Freddie Ljungberg kuwa msaidizi wangu kutokana na kutambua umuhimu wake katika ushauri na usaidizi wa kazi, ninatarajia tutafanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mkubwa ili tufaulu mtihani wa kuiweka pazuri Vfl Wolfsburg.

Jonker ambaye alikuwa kocha msaidizi wa kikosi cha mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich kati ya 2009 na 2011, aliwahi kufanya kazi na Ljungberg jijini London kwenye kituo cha kuendeleza na kuwakuza vijana cha Arsenal.

Ljungberg anaendelea kukumbukwa na mashabiki wa Arsenal, kutokana na mchango mkubwa alioutoa wakati klabu hiyo ilipotwaa ubingwa wa ligi ya nchini England bila kufungwa, msimu wa 2003-04.

Dogo Janja amtumia ujumbe mzito Makonda
Ralph Krueger: Virgil van Dijk Hauzwi