Shirikisho la soka nchini Ecuador limemfuta kazi kocha Gustavo Quinteros, kutokana na mwenendo wa timu yao ya taifa, ambayo inawania nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za 2018 kule nchini Urusi.

Kikosi cha Ecuador kilifungwa mabao mawili kwa moja na Peru juma lililopita, na kwa sasa kinashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa kundi la ukanda wa Amerika ya kusini, huku mizunguuko miwili ikisalia.

Timu nne za mwanzo katika msimamo wa kundi hilo zitakata tiketi ya moja kwa moja kushiriki fainali za kombe la dunia, huku timu itakayoshika nafasi ya tano itacheza mchezo wa mtoano dhidi ya mshindi wa ukanda wa Oceania ambaye ni New Zealand.

Shirikisho la soka nchini Ecuador tayari limeshajaza nafasi ya mkuu wa benchi la ufundi kwa kumtangaza aliyekua beki wa Bolivia Jorge Celico kuwa mbadala wa Gustavo Quinteros.

Kazi kubwa ya Celico ni kuhakikisha Ecuador inapambana katika michezo miwili iliyosalia ili kupata nafasi ya kucheza mchezo wa hatua ya mtoano dhidi ya New Zealand ili kufanikisha mpango wakufuzu na kwenda Urusi.

Jukumu la kwanza kwa kocha huyo litakua mjini Santiago, ambapo Chile wataikaribisha Ecuador mwezi ujao kabla ya kuwakabili Argentina mjini Quito.

Endapo Ecuador watashinda michezo hiyo miwili, watafanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne ama ya tano kwenye msimamo wa kundi wa ukanda wa kusini mwa Amerika.

Watu wawili wauawa na jeshi la polisi
TCRA yaja na mwarobaini kudhibiti wapotoshaji mtandaoni