Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema anatarajia Mchezo wenye upinzani mkubwa kutoka kwa Ruvu Shooting kesho Jumamosi (Novemba 19), kutokana na wapinzani wake kuwa na kikosi imara. kinachoongozwa na Benchi la Ufundi lenye weledi.

Simba SC kesho itakua Mgeni wa Ruvu Shooting katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikizitaka alama tatu sawa na wenyeji wao, ili kujiimarisha katika Msimamo wa Ligi Kuu.

Kocha Mgunda amesema amekiandaa vizuri kikosi chake kuelekea katika mchezo huo, na anaamini Wachezaji wake watapambana vilivyo ili kuiwezesha Simba SC kupata matokeo mazuri.

“Mchezo wa Kesho ni muhimu na mgumu, Ruvu Shooting ina mwalimu ambae ana sifa za kutosha, Mchezo utakuwa wa ushindani na matayarisho yote ya kucheza mchezo kama huo yamekamilika.”

“Moja ya Fair Play ni kumuheshimu mpinzani wako, ukija na matokeo yako unakuwa unamkosea heshima mpinzani wako. Na hakuna mtu anaependa matokeo mazuri kama mwalimu.” amesema Mgunda

Katika hatua hatua nyingine Kocha Mgunda amekiri kikosi chake kukabiliwa na changamoto ya kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini umaliziaji kwa wachezaji wake umekua shida.

Amesema changamoto hiyo ameifanyia kazi na anatarajia kesho Wachezaji wake wataonyesha mabadiliko kwa vitendo na kuipa timu matokeo mazuri.

“Ni kweli hatutumii nafasi nyingi tunazozitengeneza, mimi na technical benchi tunalifanyia kazi na hilo ndilo eneo tunalolifanyia kazi.” amesema

Simba SC inaelekea kwenye mchezo huo ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa ikiwa na alama 24, ikitanguliwa na Azam FC yenye alama 26 sawa na Young Africans inayopepea kileleni.

Wenyeji Ruvu Shooting wapo katika nafasi ya 13 wakiwa na alama 11 walizozipata kwenye Michezo 12 waliocheza hadi sasa, wakishinda mitatu, wakidroo miwili na wameshapoteza saba.

DART kuongeza wigo wa usafirishaji nchini
Injinia Hersi atuma ujumbe mzito CAF