Kaimu Mwenyekiti wa Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC, Mwina Mohamed Seif Kaduguda maarufu kama ‘Simba wa Yuda’ amesema Bilioni 20 za mwekezaji wa timu hiyo Mohammed Dewji “Mo” tayari zilishatolewa.

Kaduguda ameyasema hayo kufuatia kuibuka kwa maneno yanayoendelea kutolewa na wadau mbalimbali wa soka kutaka kufahamu kama je fedha hizo Bilioni 20 kutoka kwa mfadhili huyo wa Simba SC, Mo zimeshatoka ama laa.

“Mimi kama Kaimu Mwenyekiti wa Simba SC ninawaomba waandishi wa habari watusaidie ‘transformation’ ya Simba Sports Club ifanikiwe. Kwa sababu Simba ndiyo klabu pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyothubutu kufanya mabadiliko,” amesema Mwina Kaduguda.

‘Simba wa Yuda’ ameongeza ”Ukanda wote huu wa Afrika Mashariki na Kati unaiangalia Simba, je itafanikiwa ?, kwa sababu hakuna binadamu anapenda kuiga kitu kilichofeli, watu wanataka kuiga kitu kilichofanikiwa.”

“Simba ikifanikiwa itakuwa imeonyesha mwanga, imeonyesha mfano mzuri kwamba kumbe kutoka huku kuendesha mpira kwa mazoea, kwenda kuendesha mpira kwa utaratibu wa kisayansi unaotakiwa utakaoleta tija inawezekana.”

“Zile Bilioni 20 sio tatizo kubwa kwa Mohammed (Mo) kwa uwezo alionao, kwa uwezo alionao Bilioni 20 ni kitu gani kwake, Mo anauwezo. Kama kuna jambo baya Simba, mimi nitawaambia Wanasimba, lakini mabadiliko yanataka subira, yanataka utulivu yanataka uvumilivu, yanataka muda sio kitu cha mara moja.”

“Mohammed (Mo) tayari ameshaweka bilioni 20, narudia tena bilioni 20 Mohammed (Mo) alishaweka, isipokuwa tatizo kubwa ni kitu kinachoitwa ‘transformation’. Yani kutoka kwenye mfumo wa Simba Sports Club ule wa Kaduguda na Dalali kuja kwenye mfumo huu wa Bodi ndiyo kitu sasa tunaangaika nacho na lazima tufanikiwe, hilo ndiyo tatizo kubwa.”

Ikumbukwe kuwa Mo Dewji amekua mwanachama, mfadhili na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa miamba hiyo ya soka Tanzania Bara.

Kituo cha magonjwa ya mlipuko kujengwa ndani ya miezi mitatu Tanzania
Video: CAG afichua matatizo sekta ya maji