Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa Jeshi hilo linaendelea kumshikilia mwanamuziki, Vanessa Mdee kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Sirro ameeleza kuwa Jeshi hilo ambalo linamshikilia mwanamuziki huyo tangu Jumatano wiki iliyopita, linamshikilia pia mwanamuziki Rummy Shaeli na wengine kwa tuhuma hizo.

“Juzi tulimkamata Vanesa Mdee na pia tunamshikilia Rummy Shaeli,” alisema Kamanda Sirro.

“Taarifa zinaonyesha ni watumiaji na wasambazaji lakini upelelezi unaendelea na ukikamilika tutawafikisha mahakamani au tutamuachia,” aliongeza.

Kamanda Siro alifafanua kuwa Jeshi hilo pia linawashikilia baadhi ya watu na inaendelea kuwasaka wengine ambao wanasadikika kuwa hujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwenda nchini Afrika Kusini.

Vanessa alikuwa miongoni mwa majina zaidi ya 60 yaliyotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama watuhumiwa wanaojihusisha na dawa za kulevya, na kutakiwa kujisalimisha kwa jeshi la polisi. Vee Money ambaye alikuwa Afrika Kusini, alirejea hivi karibuni na kujisalimisha Jumatano ya wiki iliyopita.

‘Majina ya Wasaliti’ yavipa wakati mgumu vikao Kamati za CCM Dodoma
Kenya waomba kuwaajiri madaktari kutoka Tanzania