Rais John Magufuli ameanza kazi kwa kasi na kufanya maamuzi ambayo yanawashtua wengi na kuwafurahisha huku Watanzania wengi wakisifia maamuzi hayo na kusema ‘Huyu ndiye Magufuli, Hapa Kazi Tu’.

Moja kati ya maamuzi ambayo yamewagusa wengi, ni uamuzi alioutangaza jana wa kupiga marufuku safari zote za nje kwa watumishi wa serikali hadi pale atakapoamua vinginevyo huku akikazia kuwa mwenye uwezo wa kutoa maamuzi kuhusu masuala hayo katika serikali ya awamu ya Tano ni yeye (Rais Magufuli) na Makamu wake, Samia Suluhu.

Taarifa zilizotolewa jana na Ikulu kwa vyombo vya habari zilieza kuwa Rais Magufuli alitoa uamuzi huo baada ya kufanya kikao na Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Manaibu wao, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rished Bade.

Rais Magufuli Kikao

Alisema kuwa kazi zote zinazohusu uwakilishi wa Tanzania nje ya nchi zitafanywa na waziri wa mambo ya nje pamoja na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi husika.

Rais alieleza kuwa hivi sasa watendaji wa serikali wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kutembelea vijiji mbalimbali kujionea changamoto zinazowakumba wananchi mbalimbali vijijini na kuzitafutia ufumbuzi.

Ni dhahiri kuwa uamuzi wa Rais umelenga katika kupunguza matumizi yasio ya lazima kwa serikali kwani safari za nje (zinazotumia fedha za serikali) huongeza kwa kiwango kikubwa mzigo kwa serikali. Hii ilipigiwa kelele hasa na wapinzani katika serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo, inawezekana kuwa Rais amesitisha safari hizo ili afanye upembuzi na upekuzi wa mafaili kujua safari ipi ni ipi. Hii ni kwa sababu zipo safari nyingi zenye tija zinazofanywa na watumishi wa umma kwa kutumia bajeti ya misaada ya mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa shughuli husika ya kimaendeleo.

Mfano, misaada ya watu wa Marekani (USAID) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo hutoa fedha kwa ajili ya kuwapeleka watumishi nje wakajifunze mambo mbalimbali katika kujiongezea uzoefu na weledi katika kazi zao. Safari hizo huwa hazigusi kabisa pesa ya serikali na endapo shughuli iliyopangwa na mashirika hayo itaahirishwa na Taasisi husika basi pesa hizo hulazimika kurudishwa kwa wafadhili hao.

Pamoja na hayo yote, uamuzi huo wa Rais Magufuli ni habari njema zaidi kwa wananchi wa maisha ya chini wanaoishi zaidi vijijini. Upo uwezekano mkubwa kwa maendeleo ya vijiji mbalimbali kwani wafanya maamuzi watakuwa wanajua uhalisia wa maisha ya watanzania hao.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umekuja siku moja baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Wizara ya Fedha (HAZINA) na kukuta wafanyakazi 6 wa ofisi moja hawako ofisini. Uamuzi huo uliwashtua watumishi wengi wa umma hasa ambao ofisi zao ziko Posta, Dar es Salaam ambapo ni karibu kabisa na makazi ya Rais Magufuli (Ikulu) kwani wanaamini sasa anaweza kuwatembelea muda wowote.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwataka TRA kuhakikisha kuwa wanakusanya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa na kutosamehe kodi kwa wale ambao hawastahili kupata msamaha kwa mujibu wa sheria. Alisema uamuzi wa kusamehe kodi utatolewa na yeye mwenyewe pamoja na Makamu wake.

Rais Magufuli hakuiacha nyuma sekta ya manunuzi ya umma ambayo inatumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya serikali. Aliwaonya wale wote wanaoongeza bei kwenye bidhaa zinazonunuliwa na serikali kuacha mara moja.

“Ikitokea suala hilo likagundula kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja,” Rais Magufuli alisema.

Kasi hiyo ya Rais Magufuli inaungwa mkono na watanzania wengi wapenda mabadiliko ambao wanaimani kubwa na uongozi wa serikali hii huku wakisubiri kwa hamu kuliona Baraza lake la Mawaziri, ikiwa ni siku chache baada ya kumteua Geoge Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hakika, kasi hii itawanyoosha vilivyo watumishi wazembe na wale waliokuwa wanajipangia safari za nje kwa maslahi binafsi kwa kutumia rasilimali za serikali. Rais Magufuli ameanza vizuri, mwanzo mzuri huashiria mwisho mzuri. Kila la Kheria Rais Mchapakazi, “Hapa Kazi Tu. “

Ukawa, Polisi Watofautiana Tena
Perez Kuingia Vitani Dhidi Ya Benzema