Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila ametoa sababu za kikosi chake kushindwa kuunguruma mbele ya Simba katika mchezo wa mzunguuko wa 22 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliochezwa jana kwenye uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.

Katika mchezo huo Mtibwa Sugar walikubali kichapo cha bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi katika dakika ya 23, na kuiwezesha klabu yake ya Simba kuendelea kukaa kileleni kwa kufikisha point 52.

Katwila amesema vijana wake walicheza vizuri katika mchezo wa jana dhidi Simba lakini walikosa bahati ya kufunga.

“Kwa yoyote aliyeangalia mechi atakubaliana nami kuwa wachezaji walifanya kazi kubwa ni bahati tu haikuwa upande wetu ila tunajipanga kwa mechi zijazo.

“Simba walitumia vema nafasi waliyopata wakatufunga ila kimchezo tuliwazidi sehemu kubwa,” alisema Katwila.

Hata hivyo Katwila amesema kipigo hicho hakiwezi kurudisha nyuma morali ya wachezaji wake, badala yake watajipanga kwa mechi zijazo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo.

Wakati huo huo kikosi cha Mtibwa Sugar leos mchana kimerejea Manungu Tuariani tayari kwa maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa 23 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa siku ya Alkhamis kwenye uwanja wa Manungu Complex.

Mtibwa Sugar wapo katika nafasi ya sita wakiwa na point 27, huku wapinzani wao watarajiwa Ndanda FC wakiwa katika nafasi ya kumi baada ya kufikisha point 22.

Kambi ya Twiga Stars yavunjwa
Ligi ya wanawake kuendelea mwishoni mwa juma