Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Young Africans, Cedric Kaze, anaamini kukosekana kwa wachezaji nyota wa Simba SC Clatous Chama na Luis Miquissione kwenye mchezo wa fainali uliochezwa juzi Jumatano (Januari 13), kulisaidia timu yake kutwaa ubingwa visiwani Zanzibar.

Young Africans waliibuka mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Simba SC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati 4-3, baada ya kumaliza dakka 90 bila kufungana.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema wachezaji Clatous Chama na Luis Miquissione wana hatari kubwa, na kama wangekua sehemu ya kikosi cha Simba SC kwenye mchezo wa juzi Jumatano, wangewasumbua na isingekua rahisi kwao kufikia lengo la kutwaa ubingwa.

“Nyota hao wawili ni hatari sana wakiwapo katika kikosi, ninaamini kama wangekua sehemu ya kikosi cha wapinzani wetu wangetusumbua sana, lakini imekua bahati hawakucheza.”  Amesema Kaze

Kocha Kaze akaendelea kwa kueleza mipango na mikakati aliyoitumia kwenye mchezo huo, kwa kusema aliwahimiza wachezaji wake kutowapa nafasi wachezaji wa Simba kutomiliki mpira na kuruhusu mipira ya Krosi, jambo ambalo lilifanikiwa kwa asilimia 100.

“Niliwahimiza wachezaji wangu kuwa makini na wachezaji wa Simba SC, sikihitaji kuona wanamiliki mpira ama kupiga mipira ya Krosi, Kama wangeruhusu kupiga Krosi na ingemfikia, Meddie Kagere nina imani ingekuwa hatari, maana ninavyomjua ni hatari kwa mipira ya vichwa.” amesema Kaze.

Kuhusu ubingwa walioupata, Kocha Kaze amesema ni zawadi kwa wanachama na mashabiki wa Young Africans ambao kwa muda mrefu hawajachukua kombe lolote, hivyo ni haki yao washangilie.

“Wana-Yanga wamebezwa sana na wamekuwa wanyonge kwa muda mrefu. Hawajachukua kombe lolote kwa muda sasa, kwa hiyo hili kombe ni lao na wanastahili kushangilia,” amesema Kaze.

Young Africans wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Ijumaa (Januari 15) na kupokelewa kwa shangwe na mashabiki/wanachama wao ambao walisubiri kwa muda mrefu furaha ya kuwa mabingwa.

Simba SC waliwasili jijini humo jana mchana, lakini Azam FC waliong’olewa kwenye hatua ya nusu fainali kwa kufungwa na Young Africans wamebaki Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ili kujiimarisha na hatua ya lala salama ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo itaanza tena mapema mwezi ujao.

Museveni aongoza matokeo ya awali
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 15, 2021