Kwa mara ya kwanza kocha Msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze, amefunguka kuhusu kilichomrudisha klabuni hapo, baada ya kutimuliwa mwishoni mwa mwaka 2020, kufuatia mambo kumuendea kombo msimu uliopita.

Kaze alirejea nchini juma lililopita na kutambulishwa na Uongozi wa Young Africans kama msaidizi wa Kocha Nasreddine Nabi na rasmi alianza kazi kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliowakutanisha dhidi ya Simba SC, Jumamosi (Septemba 25).

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema amerejea Young Africans kwa ajili ya kutoa mchango wa kutwaa mataji, huku akisisitiza atashirikiana kikamilifu na kocha mkuu, Nasreddine Nabi.

“Ninafuraha kubwa kuona nimerudi ndani ya Yanga nikiwa kama kocha msaidizi, hivyo malengo ya timu ndio malengo yangu pia, nipo katika sehemu ya malengo ya timu ambayo ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa ligi kuu.”

“Hivyo nikishirikiana na Kocha Mkuu, Nabi naamini malengo yatafanikiwa japo hakuna safari ambayo haina mabonde na milima, tutapambana kuhakikisha changamoto zote tunazitatua ili tufanikiwe.” amesema Kaze

Wakati Kaze akisema hivyo, Kocha wa Viungo wa Yanga, Helmi Gueldich, ametamba kuwa wana matumaini makubwa kikosi chao kitakuwa tishio zaidi msimu huu.”

“Tumefanya usajili bora kwa ajili ya msimu huu, lakini pia tuna benchi bora la ufundi hasa baada ya kuwepo maboresho kwa kuongeza baadhi ya wakufunzi akiwemo Kaze na Zahera (Mwinyi), tuna matumaini ya kuwa na kikosi tishio zaidi,” amesema Gueldich.

Wakati huo huo mapema leo Jumatatu (Septamba 27) kikosi cha Young Africans kimeondoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Kagera, tayari kwa Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2021/22.

Young Africans itacheza dhidi ya Kagera Sugar keshokutwa Jumatano (Septamba 29), katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

Serikali yatoa maagizo maegesho ya Mv Mwanza
PICHA: Young Africans yaifuata Kagera Sugar