Kocha mkuu wa klabu ya Young Africans Cedric Kaze amesema tangu ametua kikosini hapo bado hajaona mshambuliaji mbovu anayehitaji kuwekewa jitihada zaidi isipokuwa viungo.

Kaze ameeleza tatizo la washambuliaji kushindwa kufunga ni viungo wa timu hiyo kuwa na mbinu chache za kupenyeza mipira.

“Washambuliaji wakina Sarpong na Yocuba wanashindwa kufunga kwa sababu viungo wanashindwa kutimiza majukumu yao uwanjani ikiwemo kuwapa mipira mizuri ya kufunga” alisema Kaze.

Aidha, Kaze amesema anatengeneza muunganiko wa viungo wake ili waweze kufanya kazi nzuri ya kutengeneza mabao.

Kaze mpaka sasa katika mazoezi yake amekuwa akitoa msisitizo kwa wachezaji wake kucheza mpira wa haraka haraka kuelekea katika lango la wapinzani ili kupata bao la mapema.

Anaamini kwa kucheza mpira huo unakuwa unajilinda lakini pia unawapa nafasi ngumu wapinzani kufanya vizuri, badala yake unatumia makosa yao kuhakikisha unafunga.

Kaze ambaye ana uzoefu na soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, amesaini mkataba wa miaka miwili mwishoni mwa juma lililopita kuifundisha timu hiyo akitokea nchini Canada.

TMA yatahadharisha wakazi waliopo maeneo hatarishi
Jela miaka 3 kwa kufanya mapenzi na kuku