Wakili wa Mgombea urais wa Azimio la Umoja nchini Kenya Raila Odinga, James Orengo ameiambia Mahakama ya Juu kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), haiwezi kuaminiwa kufanya uchaguzi wa kuaminika nchini humo.

Orengo amesema, kuwa taasisi zote huru zinahitajika kuheshimu mamlaka ya watu, na mamlaka lazima yatekelezwe kwa mujibu wa Katiba lakini IEBC imeshindwa katika suala hili jinsi ilivyoendesha uchaguzi wa urais.

“Tuna tume ambayo imegawanyika katikati kabisa, tunazungumzia tume ambayo haifanyi kazi yake na haiwezi kufanya uchaguzi. Mnara wa Babeli umeangushwa,” amesema Orengo.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa utangazaji wa matokeo ya Urais nchini humo, Makamishna wanne wa IEBC walijitenga na matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati wakisema kwamba hawakuweza kuthibitisha nambari hizo kutokana na “kutokuwa na uwazi”.

Mwenyekiti wa IEBC, Chebukati alidai kuwa wanne hao walitaka adhibiti matokeo ili kutangaza kuwa hakuna mgombeaji urais aliyeshinda na kusukuma nchi katika uchaguzi mpya kati ya wagombeaji wawili wakuu.

Tanzania 'mstari wa mbele' maendeleo ya jamii
Billnas, Nandy rasmi sasa ni wazazi