Mabingwa wa Tanzania bara msimu 1998/99 na 1999/00 Mtibwa Sugar, wamedhamiria kupambana kufa na kupona mbele ya Young Africans kwenye mchezo wa kesho wa mzunguuko wa 37 wa Ligi Kuu Julai 22, utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mtibwa Sugar wanaonolewa na Kocha Mkuu, Zuber Katwila kwa msimu wa 2019/20 wamekua na mazingira magumu ndani ya uwanja tofauti na msimu uliopita wa 2018/19.

Kwa sasa klabu hiyo yenye maskani yake makuu Turiani, Morogoro ipo nafasi ya 14 ikiwa imejikusanyia alama 41 baada ya kucheza michezo 36 inakutana na Young Africans ambayo ipo nafasi ya pili na alama 68.

Mchezo wa duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo jijini Dar es salaam ulishuhudia Mtibwa Sugar bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji wa Young Africans David Molinga akimalizia Krosi ya Ditram Nchimbi.

Afisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa ni mchezo mgumu kwao ila watapambana kupata matokeo chanya ambayo yatawafanya wabaki ndani ya ligi.

“Tunajua ni mchezo mgumu dhidi ya Yanga ila hakuna namna lazima tupambane tupate matokeo kama ambavyo tumekubaliana kwa pamoja, kupoteza mbele ya KMC kumetufanya tuongeze juhudi zaidi, mashabiki watupe sapoti,” amesema.

Mwishoni mwa juma lililopita Mtibwa Sugar walipoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya KMC, Uwanja wa CCM Gairo, wanakutana na Young Africans iliyotoka kulazimishwa sare ya kufungana bao moja kwa moja na Mwadui FC Uwanja wa Taifa.

CCM Kawe wamkataa Gwajima Ubunge 2020
Matokeo Majimbo 55 kura za maoni CCM