Klabu ya Azam FC imemsajili mlinda mlango kutoka nchini Uganda Mathias Kigonya kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea klabu ya Forest Rangers ya Zambia.

Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC imethibitisha taarifa za usajili wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye anakwenda klabuni hapo kupeleka changamoto kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya walinda mlango David Kissu na Benedict Haule.

Mkuu wa idara hiyo Thabit Zakaria amesema baada ya mlinda mlango huyo kukamilisha taratibu za kupimwa afya na kusaini mkataba jana Jumatano (Januari 13) akiwa jijini Dar es salaam, leo alhamisi (Januari 14) anatarajiwa kuelekea Zanzibar kujiunga na wachezaji wenzake walioweka kambi visiwani humo.

“Baada ya Azam FC kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021, timu imebaki Zanzibar kwa ajili ya kambi hadi Januari 22, hivyo Kigonya atajiunga na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu itakayoendelea baada ya fainali za CHAN.”

“Tukiwa hapa Zanzibar kikosi chetu kitacheza michezo mitatu ya kirafiki, na tunatarajia Kigonya atakua sehemu ya kikosi kwenye michezo hiyo ambayo itatusaidia kujiweka vyema kwa ajili ya michezo iliyosalia ya Ligi Kuu msimu huu 2020/21.” Amesema Thabit

Kigonya alikua mlinda mlango bora wa Ligi Kuu ya Zambia kwa misimu miwili (2018/19 na 2019/20), na kabla hajajiunga na Forest Rangers alikua akiitumikia Sofa Paka FC ya nchini Kenya.

Msimu wa 2016/2017 kigonya alitajwa kwenye kikosi bora cha Ligi Kuu ya nchini Kenya, na katika msimu huo alifunga mabao manne.

Young Africans wafichua siri ya kuidhibiti Simba SC
Hati hati Trump kugombea urais tena 2024