Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Tuisila Kisinda amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya sakata lake la usajili ndani ya Young Africans kuwekwa sawa juma lililopita.

Kisinda aliingia majaribuni, baada ya usajili wake kutoka RS Berkane kujiunga Young Africans kukataliwa na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kufuatia kanuni za usajili wa Wachezaji 12 wa Kigeni kumbana, lakini alibahatika kuingizwa katika usajili wa Mabingwa hao kutokana na kuondoka kwa Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Lazarius Kambole kutimkia Uganda.

Kiungo huyo amesema alifuarahishwa na maamuzi ya kukubaliwa kuwa sehemu ya wachezaji wa Young Africans, na sasa anajiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Nimefurahi kuona kila kitu kimemalizwa vizuri na Uongozi wangu, nilikuwa na hofu huenda kungekuwa na ugumu kufuatia sintofahamu iliyotokea kwenye usajili wangu.”

“Nimejiunga na wenzangu na tayari ninaendelea na Program za pamoja za kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.” amesema

Katika hatua nyingine Kisinda amesema ana deni kubwa kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Africans, hivyo hana budi kuipambania timu yao na kuipa matokeo.

Kuhusu mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Mchezaji huyo amesema yupo tayari kuikabili Al Hilal ya Sudan inayonolewa na Kocha wake wa zamani Florent Ibenge, ambaye alifanya naye kazi akiwa AS Vita ya DR Congo kisha RS Berkane ya Morocco.

“Nina deni kubwa kwa wanayanga ambao wanatarajia mazuri kutoka kwangu nimefanya kazi na Florent Ibenge msimu uliopita, kila mmoja anafahamu ubora wa mbinu zake, lakini wakati huu ni Young Africans dhidi ya Al Hilal, lazima nipambane kuhakikisha timu yangu inafika hatua ya makundi.” amesema Kisinda

Young Africans itacheza na Al Hilal kati ya Oktoba 7-9, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na itamalizia ugenini mjini Omdurman-Sudan kwa kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Oktoba 14-16.

Ikiwa Young Africans itaitoa Al Hilal na kufuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, itajihakikishia kitita cha fedha kiasi cha Dola za Marekani 550,000 sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 1.3 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Na kama itatokea Young Africans inatolewa katika hatua hiyo, itaangukia hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, endapo itafuzu hatua ya Makundi itajihakikishia Dola za Marekani 275,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 641 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Wanne wasimamishwa kazi kupisha uchunguzi mil. 300
Ally Mayay: Nilishtushwa na uteuzi, nimesikia maagizo ya waziri