Kocha Mkuu wa Young Africans Nassredine Nabi amewatoa wasiwasi baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kwa kusema haihofii Al Hilal ya Sudan, baada ya kufanikisha mpango wa kuing’oa Zalan FC ya Sudan Kusini.

Young Africans itacheza na Al Hilal kati ya Oktoba 7-9, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na itamalizia ugenini mjini Omdurman-Sudan kwa kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Oktoba 14-16.

Nabi amesema yupo tayari kwa mchezo huo na kwa maandalizi atakayoyafanya katika kipindi hiki, yatakiwezesha kikosi chake kupambana vilivyo katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza ili kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya kwenda Ugenini kwa ajili ya Mkondo wa Pili.

Amesema hadi sasa ana taarifa za kutosha kuhusu Al Hilal na ameanza kuzifanyia kazi kimkakati.

“Tunajua uzuri na ubovu wao uko wapi, tutafanya maandalizi ya kupambana na kwa mujibu wa tulichokua nacho katika kipindi hiki, Young Africans inapigania heshima yake na ya nchi ya Tanzania kwa ujumla, hivyo hatutakua tayari kupoteza kwenye mchezo huo.”

“Hali kadhalika hata sisi tunajua Al Hilal nao wana taarifa zetu na wameshaanza kuzifanyia kazi, lakini hilo bado halinitishi kwa sababu lengo ni kupambana na kufanikisha mpango wetu.” amesema Nabi

Ikiwa Young Africans itaitoa Al Hilal na kufuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, itajihakikishia kitita cha fedha kiasi cha Dola za Marekani 550,000 sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 1.3 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Na kama itatokea Young Africans inatolewa katika hatua hiyo, itaangukia hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, endapo itafuzu hatua ya Makundi itajihakikishia Dola za Marekani 275,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 641 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

EWC yasema Elimu haiwezi kusubiri majanga
Ruto kuhutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa