Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddine Nabi ameibuka na kuwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya wao kushindwa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika huku akitamba watakachokutana nacho wapinzani wao ambao watapambana nao watasimulia.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo baada ya kushuhudia timu hiyo ikishindwa kubebe taji hilo mbele ya USM Alger ya Algeria licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao juzi Jumamsi (Juni 03).

Kocha huyo alisema mashabiki wanapaswa kumsamehe yeye na vijana wake kwa kuwa wameshindwa kutimiza lengo ambalo walikuwa wanaweza kulifikia kama wangefanya kazi ya ziada.

Nabi alifunguka kuwa, anafahamu namna ambavyo mashabiki wamevunjika moyo kwa hatua hii ya Young Africans ya kukosa ubingwa, ila ana imani wataendelea kuwa sehemu ya faraja kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa kuwa bado wana fainali nyingine mbele yao.

“Niwaombe radhi mashabiki wa Young Africans kwani kwa hakika walistahili furaha zaidi, walistahili kuwa na kitu cha kujivunia msimu huu.

“Walikuwa nasi kwenye kila nyakati lakini wameshindwa kufurahia kuwa mabingwa wa Afrika. Imani yangu na wachezaji ni kwamba bado watakuwa nasi kwenye mchezo mwingine wa fainali uliopo mbele yetu na mechi mbili za kumalizia ligi ya msimu,” alisema Nabi.

Timu hiyo imetwaa ubingwa wa Tanzania Bara ikiwa na alama 74 baada ya kucheza mechi 28 kwenye ligi na imepoteza mechi mbili pekee dhidi ya Ihefu na Simba SC.

Mechi mbili ambazo zimebaki ni dhidi ya Mbeya City inayotarajiwa kuchezwa Juni 6 na ile dhidi ya Tanzania Prisons ambayo inatarajiwa kuchezwa Juni 9.

Okrah afunguka ya moyoni Simba SC
Mhubiri Mackenzie awadai Wanahabari mgao wake