Kiungo kutoka nchini Croatia Mateo Kovacic amemtaka meneja mpya wa klabu ya Real Madrid Julen Lopetegui kumpa baraka za kuihama klabu hiyo, ili apate nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Kovacic ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Croatia kilichofika fainali ya michuano ya kombe la dunia, amewasilisha ombi hilo kwa kuamini huenda meneja huyo mpya akaafiki, kutokana na kuchoshwa na hatua za kuwekwa benchi na kutumika kama mchezaji wa akiba.

Uwepo wa wachezaji Casemiro, Luka Modric na Toni Kroos umekua kikwazo cha kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24.

“Ningependa kucheza mara kwa mara, ili kutunza kipaji changu, nimekua sipati nafasi hiyo Real Madrid, ninaamini kama nitafanikiwa kuondoka nitafikia lengo la kucheza kila mwishoni mwa juma,” alisema Kovacic alipozungumza na mwandishi wa habari wa gazeti la Marca la Hispania.

“Nafahamu kwa sasa ni vigumu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, lakini nikiondoka ninaamini nitafanikiwa kupata nafasi hiyo.

“Umri wangu bado mdogo, ninahitaji kucheza, kama ilivyo kwa wachezaji wengine wenye umri kama wangu ambao kila mwishoni mwa juma wamekua wakipatiwa nafasi ya kuvitumikia vikosi vya klabu zao, na wanafanya vizuri.”

Tayari klabu za Manchester City, Bayern Munich, Juventus na Manchester United zinatajwa kuiwania saini ya Kovacic, ambaye thamani yake  inakadiriwa kufikia Pauni milioni 80.

Rais Magufuli akabidhiwa Bilioni 723 gawio la serikali
LHRC yampinga waziri Lugola suala la kulaza madereva mahabusu

Comments

comments