Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta, amewasili nchini Tanzania na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa ziara binafsi ya siku mbili.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuwasili wilayani Chato mkoa wa Geita, Kenyatta amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu hivyo hakuna haja ya kuzuia kutembeleana na kufanyabiashara kwa pamoja.

Amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanapaswa kupuuzwa kwani wamekuwa wakijisahau na kutoa matamshi ambayo yanaashiria chuki na ubaguzi baina ya wananchi wa nchi za Afrika Mashariki.

”Kuna watu wanaropoka huko. Unawezaje kuzuia Mtanzania asifanye biashara Kenya au Mkenya asifanye Biashara Tanzania? Tunataka kushirikiana na kuona ushirikiano unakua na ndio maana tumeona sio kila siku ziara za Kitaifa, leo nataka nikale Sato nyumbani kwa Rais Magufuli,”amesema Rais Uhuru Kenyatta

Kwa upande wake, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesisitiza upendo, umoja na ushirikiano baina ya raia wa nchi za Afrika Mashariki, kwani kufanya hivyo kutaongeza kasi ya maendeleo katika ukanda wa nchi hizo.

Hata hivyo, hivi karibuni mbunge wa jimbo la Starehe lililopo Nairobi nchini Kenya, Charles Kanyi maarufu kwa jina la ‘Jaguar’ alitoa matamshi ambayo yalikuwa yakiashiria ubaguzi kwa raia wa kigeni nchini humo wakiwemo Watanzania, akitaka waondolewe.

 

Vanessa Mdee arusha jiwe gizani, ni kwa Jux?
Video: Naibu Waziri atembelea banda la Maliasili na Utalii | Ataja Magoroto, Magamba | Fursa kwa Watanzania

Comments

comments