Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameeleza ya moyoni kuhusu maisha aliyokutana nayo ikiwa ni takribani miezi 18 tangu alipohama CCM na kujiunga na Chadema akipewa nafasi ya kugombea urais mwaka jana.

Lowassa ambaye ni mwanasiasa mkongwe ameeleza kuwa baada ya kuhamia Chadema hakutegemea kukutana na changamoto alizokutana nazo.

“Niseme maisha nje ya CCM yana changamoto zake. Sikutegemea kama kungekuwa na chamangamoto namna hii,” Lowassa anakaririwa na Mwananchi.

Aliongeza kuwa changamoto alizozipata zipo nzuri na mbaya lakini anaamini kuwa amesaidia kuwapa nguvu baadhi ya watu kwa kuamini wanaweza kufanya vizuri zaidi na wanaweza kusema.

Aidha, Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema kuwa hafurahishwi na baadhi ya mambo yanayofanywa na vyama vingine vya siasa pamoja na vyombo vya dola. Alisema kuwa baadhi ya watu waliomuunga mkono katika uchaguzi uliopita wamekuwa wakisumbuliwa.

Hata hivyo, Lowassa amesema kuwa anafurahishwa na jinsi ambavyo Chadema inavyongozwa chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na kwamba wataendelea kufanya mikutano ya ndani nchi nzima kuhakikisha wanaendelea kukiimarisha chama hicho.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliinyoshea kidole CCM akidai kuwa imekuwa ikirudi nyuma badala ya kwenda mbele kwa kukosa uvumilivu dhidi ya vyama vya upinzani.

“Nasikitika chama hiki cha CCM kimerudi nyuma badala ya kwenda mbele kutokana na kutovumilia upinzani. Baya zaidi ninaloliona ni kuwanyima watu haki ya kushiriki katika mazungumzo yao,” alisema.

Lowassa ameeleza pia kuwa kutokana na kuwepo na siasa za chuki zinazoendeshwa na baadhi ya watu, yeye pamoja na viongozi wengine wa vyama vya upinzani akiwemo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wamekubaliana kubeba ajenda ya umoja na ushirikiano.

Alisema kuwa anachokiomba kwa Mwaka 2017 ni kuheshimiwa kwa demokrasia nchini pamoja na kutowanyanyasa watu wanaoamini tofauti, hasa wanaounga mkono vyama vya upinzani.

Lowassa alisema kuwa anafurahishwa na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini na kwamba itaendelea kuwa hivyo kwakuwa vyama vya upinzani vinaendesha siasa zao kistaarabu.

Mzee Kingunge aeleza kwanini Wapinzani hawatashinda 2020 kwa hali hii
Video: Yatambue maua yenye sumu msimu huu wa Christmas