Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, jana aliweka wazi jinsi alivyoweza kumshawishi Muhubiri maarufu kutoka nchini Nigeria, T.B Joshua kutohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais John Magufuli, ingawa aliletwa nchini na CCM.

Akizungumza jana katika mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wafuasi wa Chadema (Chaso), Lowassa ambaye alieleza kuwa ni rafiki wa karibu wa T.B Joshua wa Synagogue Church Of All Nations (SCOAN), alisema kuwa CCM ndio waliomualika mhubiri huyo kuja nchini kwa lengo la kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Magufuli na kumshawishi [Lowassa] akubaliane na matokeo ya uchaguzi huo.

“Walimuita rafiki yangu TB Joshua, wakaenda wakampokea. Alipokelewa na Rais Magufuli, akapelekwa Ikulu akazungumza na Kikwete. Baadaye akawaambia wamlete kwangu. Kweli akaja nyumbani kwangu, tukazungumza naye. Sitaki kusema mengi sana niliyomwambia, lakini moja, nilimwambia ukikubali yale matokeo ndugu yangu, heshima yako itashuka hapa nchini na duniani kwa ujumla,” Lowassa anakaririwa.

TB Joshua na Dk Kikwete

Lowassa alieleza kuwa yeye pamoja na viongozi wengine wa Ukawa walikutana na T.B Joshua na kumueleza kuhusu uchaguzi ulivyoendeshwa na alikubaliana nao. Kutokana na kukasilishwa na maelezo hayo, Mhubiri huyo alibadili utaratibu aliokuwa ameandaliwa na wenyeji wake na kuendelea na utaratibu wake kabla hajaondoka nchini bila kuhudhuria tukio hilo la kihistoria (Novemba 4, 2015).

TB Joshua

Mwanasiasa huyo mkongwe alielendelea kusisitiza kuwa alishinda uchaguzi uliopita lakini ushindi wake uliporwa na CCM.

“Tulishinda vizuri sana lakini hata hizo walizotupa, zinatosha kuwaambia kuwa tuliwapa kazi ya kutosha. Nyie mnajua, wao wanajua na mimi najua,” alisema.

T.B Joshua aliingia nchini Novemba 3 mwaka jana na kupokelewa na Rais John Magufuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kisha kuelekea Ikulu ambapo akikutana pia na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na viongozi wengine.

Baadae, Mhubiri huyo alionekana akiwa na viongozi wa Ukawa nyumbani kwa Lowassa na kufanya ibada maalum siku iliyofuata kabla ya kuondoka nchini, matukio ambayo yaliacha maswali mengi kwa wafuatiliaji.

Mwaka 2011, Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, alienda Nigeria na kuhudhuria idaba katika kanisa la T.B Joshua na baadae yeye na familia yake walikutana na Mhubiri huyo na kupiga picha kadhaa zilizoonekana kwenye mitandao ya kijamii. Mwaka 2012, Lowassa pia alihudhuria ibada katika kanisa hilo akwia na mkewe na walifanya hivyo mara kadhaa. Mwingine aliyewahi kuhudhuria ibada katika kanisa hilo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alionekana katika kanisa hilo.

Video: Watatu wamepoteza maisha baada ya kula mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu, Morogoro
CCM yataja tarehe rasmi ya kumkabidhi Magufuli Uenyekiti