Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, kuunda Kamati Maalum ya kuchunguza tukio la kupigwa kikatili na Polisi Loliondo, Mkazi wa Namanga Mkoani Arusha.

Tukio hilo la kijana huyo, Mussa Yahya ambaye alikuwa na wenzake watano, wanatuhumiwa kuiba vitu vya wageni katika kambi ya kitalii iliyopo wilayani Ngorongoro Mkoani humo, na kupelekea kushikiliwa na askari polisi ambao wanalalamikiwa kuwapiga na kuwafanyia vitendo vya kikatili vilivyopelekea kuoza mguu wake wa kushoto.

Akiwa katika ziara Wilayani Longido, na kufanya mkutano wa hadhara mjini Namanga, kijana huyo ambaye aliambatana na kaka yake, alimweleza Waziri Lugola katika mkutano huo,  alipigwa na kuteswa kwa siku tisa huku yeye na wenzake wakiwa wamefungwa mikono na miguu huku wakiwa wanapigwa katika nyayo za miguu hadi kupelekea mguu wake kuoza.

“Nikiwa mimi na wenzangu, baada ya kuteswa na askari hao, tukapelekwa hospitali, na baada ya vipimo, ndipo mimi nikaambiwa na madaktari mguu wangu umeoza na wakakata nyama ya mguu wangu, nimepata mateso sana, pia walinifanyia ukatili sehemu za siri kwa kuniingizia chupa,” amesema Yahya.

Aidha, kufuatia malalamiko hayo pamoja na kaka yake, Omary Yahya ambaye aliambatana naye katika mkutano huo wa Namanga, Waziri Lugola alimaliza ziara Wilayani Longido na kuelekea Wilaya ya Karatu na baadaye akafika Wilaya ya Ngorongoro mahali ambapo tukio hilo la kupigwa kwa kijana huyo lilitokea.

Akizungumza na wananchi mjini Waso, Loliondo, Wilayani Ngorongoro, Lugola amesema kuwa kutokana kwa tukio hilo la kikatili lililotokea wilayani hapo, alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuhakikisha unafanyika uchunguzi huru ili haki itendeke kwani wananchi wamelalamika juu ya tukio hilo.

“Nilipata malalamiko haya nikiwa Namanga kutoka kwa aliyejeruhiwa, na nilimuona majeraha yake jinsi alivyokuwa ameteswa, hivyo basi ili nijue ukweli zaidi wa tukio hili, namuagiza Katibu Mkuu aunde Kamati kwa ajili ya kuchunguza kwa kina kuhusu tukio hili,” amesema Lugola

Hata hivyo, ameongeza kuwa tayari alishatoa maagizo kuwa, mahali popote polisi wakikutana na jambazi lenye silaha ya moto lazima askari ajihami kwa kupambana na jambazi huyo mwenye silaha, ili askari huyo asiweze akaja kupoteza Maisha wakati anacho kitu cha kujihami.

 

Rais Dkt. Shein aweka wazi msimamo wake kuhusu uchaguzi Zanzibar
Walimu wajitolea kujenga darasa