Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka askari pamoja na watumishi mbalimbali waliopo ndani ya Wizara yake wawe huru kuuliza maswali, kusema kero zao zinazowakabili katika vikao vyake na hakuna kiongozi yeyote atakaye wanyanyasa baada ya yeye kuondoka.

Waziri Lugola amesema hayo baada ya kuona baadhi ya watumishi katika ziara mbalimbali anazozifanya nchini, wanakua na woga wa kusema kero zao wakihofia watapata matatizo baada ya yeye kumaliza kikao.

Amesema kuwa wakati anapata mambo mengi ambayo yanamsaidia kutatua kero za watumishi wake licha ya kuwa baadhi ya watumishi wanakua na woga wa kusema matatizo yanayowakabili.

Akizungumza katika kikao na askari na Maafisa wa Jeshi la Magereza wa Gereza la Kilimo la Mbigiri, liliopo Wami-Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro, jana, Lugola alisema ili aboreshe utendaji kazi wa Wizara na Idara zake, anahitaji kujua matatizo mbalimbali ya watumishi wake, hivyo katika kikao chake ruksa watumishi kuuliza maswali kwasababu kupitia maswali hayo yanamsaidia sana kutatua kero zao.

“Mimi ndio Waziri wenu, ulizeni swali lolote, toeni kero zenu na hakuna wakuwafuatilia baada ya kikao hiki, hiki ni kikao cha Waziri wenu mmepata nafasi hii ulizeni, niambieni matatizo yenu yanayowakabili ili tuyafanyie kazi,” alisema Lugola.

Pia aliwaambia watumishi hao endapo watapata matatizo baada ya kusema kero zao katika kikao chake, wawe huru kumuambia japo anaamini hakuna chochote kitakacho wakuta maana kikao chake ambacho ni huru.

Lugola aliyasema hayo baada ya baadhi ya askari wa Gereza hilo kuwa na hofu wakati walipokua wanauliza maswali ambapo mmoja wao akitoa kero yake huku akitahadharisha kuwa Waziri huyo amlinde endapo atapata matatizo mara baada ya kikao hicho kumalizika.

Hata hivyo, Lugola aliutaka uongozi wa Gereza hilo kuacha malalamiko na badala kutafuta  majibu ya changamoto zinazowakabili na pia wahakikishe wanasimamia nidhamu kwa askari na kutooneana, na pia waendelee kutumia vitendea kazi vilivyopo katika Gereza hilo ili waweze kuongeza uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo, (ACP) Shija Fungwe, alimshukuru Waziri Lugola kwa kufanya ziara katika Gereza lake, na pia maagizo yake aliyoyatoa watayafanyia kazi likiwemo la kuongeza uzalishaji kupitia vitendea kazi walivyonavyo na pia yeye pamoja na askari na Maafisa mbalimbali wa Gereza hilo aliweka wazi kuwa wanaishi vizuri, kwa ushirikiano na pia wapo huru kuzungumza naye kuhusu jambo lolote la utendaji kazi.

 

Hata hivyo, Waziri Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo ambalo linafanya shughuli za kilimo ya mazao mbalimbali pamoja na ufugaji  wa ng’ombe, kondoo, mbuzi na kuku ambapo kwa ujumla wana mifugo zaidi ya 1000.

 

LIVE BAGAMOYO: Maadhimisho ya Miaka 150 ya UINJILISHAJI Tanzania
Mradi wa TACIP wamkuna RC Makonda, aahidi ushirikiano