Serikali visiwani Zanzibar imeyafungukia maduka matatu makubwa  wilayani Wete ambayo yalibainika kufanya ubaguzi kwa kutowahudumia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid amewaambiwa waandishi wa habari kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kina, walibaini kuwa wafanyabiashara Said Juma Seif, Titi Juma Othman na Hamad Haji wanaomiliki maduka makubwa hukataa kuwahudumia wanaCCM.

“Tumelazimika kuyafungia maduka hayo matatu baadaya Serikali ya Walaya kujiridhisha kuwa yanawabagua wanachama wa CCM,” Rashid anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amefunga biashara ya magari yote yanayobeba abiria katika barabara ya Wete – Mtambwe akieleza kuwa amebaini yanawabagua wana CCM. Pia, alieleza kuwa Serikali ya Wilaya itasaidiana na Wizara husika kuchukua hatua zaidi.

Nao baadhi ya Madereva na Makondakta wa magari hayo walieleza kuwa wao hawawashushi abiria kwa misingi yoyote kwani wanataka pesa, lakini wananchi wenyewe wanaopanda magari hayo ndio wanaobaguana na kuwashusha wanachama wa CCM.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita ameendelea kufanya ziara yake visiwani humo akiwataka wananchi kushirikiana naye kuikataa Serikali ya Rais Ali Mohamed Shein.

“Tukikazana, serikali hii itaondoka madarakani. Ikiwa mnangoja Maalim Seif aua Marekani kuiondoa kwa sheria ya Kimataifa haitawezekana kwani Marekani haiwezi kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar,” alisema Maalim Seif katika moja ya mikutano yake.

Kwa upande wa CCM, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa hivi sasa hawana muda wa kujibizana na CUF kwa kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba watakutana tena majukwaani mwaka 2020.

FA Yabaini Kulikua Na Kasoro Za Utovu Wa Nidhamu
Video: Museveni adaiwa kumuandaa mwanae, ampaisha jeshini