Maelfu ya abiria wamekwama leo katika viwanja vya ndege vinne vikubwa nchini Kenya baada ya kushindwa kusafiri kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa viwanja hivyo.

Wafanyakazi hao wamegoma baada ya kutoridhishwa na mpango wa kuunganisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Shirika la Ndege la nchi hiyo.

Takribani ndege 60 zimeshindwa kusafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta leo, uwanja ambao ndio mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Hata hivyo, shughuli za kawaida zilirejea mchana.

Viwanja vingine vya ndege vilivyoathiriwa na mgomo huo ni pamoja na Mombasa, Eldoret na Kisumu.

Serikali ya Kenya kupitia taarifa yake kwa umma imelaani vikali mgomo huo na kuuelezea kuwa ni kinyume cha sheria. Polisi wa kutuliza ghasia walifika katika viwanja vya ndege kuwatawanya wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya mgomo na kuandamana, kwa mujibu wa Citizen.

Wafanyakazi wa ndege za jeshi walipelekwa katika viwanja hivyo na kuanza kutoa huduma kwa lengo la kuwasaidia abiria kuendelea na safari zao.

Shirika la Ndege la Kenya Airways limeeleza kuwa baadhi ya ndege zake zimefanikiwa kuendelea na safari kwenda Amsterdam na Mumbai, pamoja na safari nyingine za ndani.

Baadhi ya ndege zinazoenda nje ya bara la Afrika zimeahirisha kabisa safari zake kufuatia hali hiyo.

Umoja wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege wanapinga uamuzi wa Serikali wa kulipa Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) jukumu la kusimamia viwanja vya ndege ikiinyang’anya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) ambayo ilikuwa ikiingiza faida.

Mgeja amfuata Lowassa CCM, aiponda Chadema ‘hawashauriki’
Korea Kaskazini yadaiwa kujenga upya vinu vya nyuklia

Comments

comments