Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameeleza kushangazwa na ripoti ya polisi kuhusu sakata la kutekwa bilionea Mohammed Dewji na baadaye kuachiwa huru na watesi wake.

Akizungumza leo katika tukio la kuwaapisha mawaziri waliobadilishana ofisi, Profesa Palamagamba Kabudi (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Balozi Augustine Mahiga (Sheria na Katiba), Rais Magufuli alisema kuwa tukio la kutekwa na kuachiwa kwa mfanyabiashara huyo limeacha maswali mengi hususan kupitia taarifa zilizotolewa na jeshi la polisi.

“Kuna mambo mengine ya kawaida ambayo Jeshi la polisi inabidi muelewe, kwamba Watanzania sio wajinga sana. Wanafahamu na wanajua kuchambua mambo. Niwape mfano kidogo, alipotekwa huyu Mohammed, kulikuwa na mambo mengi, ametekwa na aina fulani ya wazungu. Lakini lilivyokuja kumalizika lile swali linaleta maswali mengi zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa ingawa ana imani kubwa na jeshi hilo, taarifa za Polisi linapaswa kujiangalia katika ripoti za matukio kama hayo.

“Mtu aliyetekwa alikutwa Gymkhana usiku, lakini watu wanajiuliza ‘aliendaje pale?’ Lakini alipowekwa pale na bunduki zikaachwa pale, watu wanajiuliza huyu mtekaji aliyeziacha… Je, angekutana na polisi wanaomtafuta njiani [ingekuwaje]? Walijaribu kulichoma gari, lakini baadaye tunamuona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa,” alisema Rais Magufuli.

Mshangao huo pia aliuelezea katika tukio la kupatikana kwa eneo ambalo Jeshi la Polisi lilisema kuwa Mo alipotekwa alikuwa ametunzwa, maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

“Baada ya siku chache tukaambiwa nyumba alimokuwa ametekwa ni hii hapa na aliyekuwa anawabeba wale watekaji ni huyu hapa. Watanzania tukawa tunasubiri kwamba huyu sasa ndiye atakuwa kielelezo cha kupeleka mahakamani tusikie kitakachotokea lakini kimya mpaka leo miezi imepita,” alieleza.

Alisema kuwa Watanzania walitegemea wangemuona hata mmiliki wa nyumba hiyo akieleza kuhusu kilichotokea kwa wateja wake lakini haikuwa hivyo.

Mo Dewji alitekwa Oktoba 11 mwaka jana katika hoteli ya Colosseum, Oyterbay jijini Dar es Salaam na kupatikana siku tisa baadaye akiwa ametelekezwa katika eneo la Gymkhanas.

Video: Msanii mkubwa apigwa na mpenzi wake chumbani akionekana InstaLive
Sumaye atoboa siri ya Lowassa kurudi CCM, 'Tunavumilia mengi'

Comments

comments