Wadau wa Mazingira  na Wazalishaji wa Mifuko ya Plastiki hapa nchini wameipongeza Serikali kwa kuwakutanisha pamoja ili kujadili kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki na kutoa maoni yao kwa Serikali juu ya kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Akizungumza wakati akifungua  kikao cha wazi cha kupokea maoni ya wadau kuhusu dhamira ya Serikali kupiga marufuku uzalishaji, uuzaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba amesema dhamira ya Serikali ni kupata maoni ya wadau na wazalishaji wa mifuko hiyo ili Serikali ifanye tathmini kabla ya kuchukua hatua na kuweka mazingira yatakayowezesha utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa kila mdau.

“Changamoto imekuwa kubwa katika matumizi ya mifuko ya plastiki katika swala la mazingira kwani tumeshuhudia miundo mbinu yetu ikiathirika, mifugo na hata viumbe vya baharini na kwa mujibu wa tafiti kuna hatari baadae mifuko hii ikawa mingi zaidi baharini kuliko samaki,” amesema Makamba.

Amesema kuwa Serikali imeona ni vyema ikakutana na wadau ili ipate maoni yao kwa kuzingatia kifungu cha 178 cha Sheria ya Mazingira kinachotaka wananchi na wadau kushirikishwa na kupata taarifa kuhusu maswala ya mazingira.

Aidha, Makamba amesema kuwa kuanzia sasa Ofisi yake itakuwa ikishirikiana na wadau katika mambo yote yanayohusu mazingira ili kuongeza tija na kutoa fursa kwa wadau hao kutoa maoni yatakayosaidia katika usimamizi wa Sheria na Kanuni.

Hata hivyo, Waziri Makamba amelitaka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia Sheria ya Mazingira kikamilifu ili kulinda rasilimali za Taifa ambazo zimekuwa zikiteketea kila siku.

Kwa upande wake Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Plastiki Tanzania, Ahmed Abdallah amepongeza utaratibu huo wa Serikali kukutana na wadau mbalimbali wa mazingira kujadili na kuangalia namna ya kutatua kero hizo.

 

Uchumi wa Korea Kaskazini wazidi kuimarika
Lukuvi awaweka kikaangoni maafisa Ardhi na Mipango