Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha kila shule ya sekondari inayojengwa inajengwa ikiwa na maabara.

Ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tano mkoani humo.

Aidha, Makamu wa rais ameanza ziara yake kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji uliopo Kiloleli ambapo mradi huo ukikamilika utasaidia kupatikana kwa maji safi na salama kwa vijiji vitatu na utagharimu shilingi za Kitanzania Bilioni 1.6 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 80%.

Vile vile, Samia Suluhu amewapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika uwekezaji na uendelezaji wa viwanda ambapo mpaka sasa kuna viwanda 14 vya usindikaji wa pamba na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mazao 1,035.

Hata hivyo, Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi hao kuwa hadi mwisho wa mwezi huu chupa milioni 2 za dawa za kuuwa wadudu wanaoshambulia pamba zitakuwa zimesambazwa.

 

Trump ataka sheria ya umiliki wa silaha ifanyiwe marekebisho
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Februari 20, 2018