Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu amewasihi Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki, ambacho wanasubiri kumtangaza Mdhamini wa Michuano ya Kimataifa.

Simba SC ni sehemu ya Klabu ambazo zinabanwa na Kanuni za udhamini wa Michuano ya CAF, ambazo haziruhusu udhamini wa Kampuni za Ubashiri, kuanzia hatua ya Makundi.

Mangungu amesema Uongozi wa Simba SC upo makini na dhamira yao kubwa ni kutaka kuendelea kuiweka Taasisi hiyo katika hali nzuri na salama, ili kupekuka Mgogoro na Mdhamini wao Mkuu Kampuni ya M-bet.

“Simba SC ni taasisi, hatutaki kuingia katika Migogoro na wadhamini wetu wakuu M-bet, hivyo tunaheshimu mkataba tulioingia, tunafanya utaratibu ambao utainufaisha Klabu bila kuathiri makubaliano yetu na Mdhamini Mkuu.”

“Ninachowaomba Wanachama na Mashabiki waendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho tupo katika hatua za mwisho kabla ya kumtangaza Mdhamini tutakayeenda naye Kimataifa.”

“Mdhamini huyo atatupatia udhamini mkubwa utakaoendana na hadhi ya timu yetu ya Simba SC, Mdhamini huyo atakaa kifuani.” amesema Mangungu

Kuhusu Mgogoro wa Kimkataba unaoendelea kwa Watani zao wa Jadi Young Africans, Mangungu amesema anaamini Mgogoro huo utakwisha kwa sababu unazungumzika.

“Tunaamini hata wenzetu wenye Mgogoro wanaweza kukaa mezani wakaelewana, haya mambo yanajadilika.” amesema Mangungu

Simba SC imekua ikitumia Udhamini wa Visit Tanzania kila inapoingia hatua ya Makundi na kuendelea kwenye Michuano ya CAF.

Precision Air warudisha shukurani Bukoka
Ratiba ya Bunge yashtua kutotaja Muswada wa Sheria ya Habari, TEF yawatuliza wadau