Mshambuliaji kutoka nchini Ujerumani Mario Gomez amekubalia kurejea katika ligi ya nyumbani (Bundesliga) baada ya kusaini mkataba wa kuitumikia klabu ya VfL Wolfsburg.

Gomez jana alisaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo kwa kuamini ni wakati mwingine kwake kurejea nyumbani ambapo ndipo alipoanzia soka kabla ya kuondoka mwaka 2013 na kutimkia nchini Italia.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, amekubali kurejea katika ligi ya Bundesliga baada ya klabu ya Fiorentina ya Italia kumpelekwa kwa mkopo nchini Uturuki katika klabu ya Besiktas ambayo aliifungia mabao 26 na kuisaidia kutwaa ubingwa wa ligi.

Uwezo wake kisoka katika ligi ya nchini Uturuki ulimuwezesha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani ambacho kilishiriki fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa.

Baada ya kumalizika kwa fainali hizo, Gomez alitangaza kutorejea tena nchini Uturuki kufuatia vurugu za kisiasa ambazo zilizoibuka nchini humo hivi karibuni kwa jaribio la kutaka kuipindua serikali.

Gomez, alianza kucheza ligi ya nchini Ujerumani akiwa na klabu ya VfB Stuttgart mwaka 2003, na aliifungia mabao 138 katika michezo 236 aliyocheza. Mwaka 2009 alihamia FC Bayern Munich kabla ya kutimkia Fiorentina mwaka 2013.

Kwa upande wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mario Gomez amecheza michezo 68 na kufunga mabao 29.

Kingsley Coman Kukaa Nje Majuma Manne Hadi Manane
Rais Magufuli ateua Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha