Aliyewahi kuwa beki wa kati wa Washika Bunduki Wa Kaskazini Mwa Jijini London (Arsenal) Martin Keown, ameutaka uongozi wa benchi la ufundi na klabu hiyo kumvua kitambaa cha unahodha mshambuliaji kutoka nchini Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, katika kipindi hiki ambacho anagomea kusaini mkataba mpya.

Mkataba wa Aubameyang utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, lakini bado hajafikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya, huku taarifa zikieleza kuwa, huenda akaachana na miamba hiyo ya Emirates.

Staa huyo wa kimataifa wa Gabon alipewa kitambaa hicho cha unahodha Novemba mwaka jana baada ya kuvuliwa kiungo Granit Xhaka kutokana na kitendo chake cha kuwajibu kwa hasira mashabiki wa timu hiyo ya Arsenal waliokuwa wakimzomea.

Kuhusu shughuli ya ndani ya uwanja, Aubameyang ameonyesha kuwa ni moto, akifunga mabao 49 katika mechi 75 alizocheza kwenye Ligi Kuu England, lakini Keown anaamini kwamba mchezaji huyo anapaswa kunyang’anywa unahodha.

 “Nadhani meseji inapaswa kutumwa kwa mchezaji kwamba hawezi kuwa nahodha wakati mkataba wake ukiwa na shaka kubwa, huu ni mwaka wa mwisho wa mkataba wake na hilo halipaswi kuachwa liendelee kutokea.” Amesema Keown.

Keown anaamini kwamba Aubameyang ataachana na klabu hiyo wakati wa dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa huku Real Madrid ikihusishwa zaidi na mpango wa kunasa saini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

“Nadhani ataondoka akiwa na moyo mweupe kabisa,” alisema beki huyo wa zamani wa England.

Hata hivyo, Keown amewaambia mabosi wa klabu hiyo kufikiria uwezekano wa kumbakiza Aubameyang kwenye kikosi chao hata kama ataondoka bure kwa sababu hilo litawafanya kuwa na uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.   

Taharuki Mbowe kushambuliwa, Kamanda Muroto athibitisha
Serikali yaagiza Chuo cha Diplomasia kuongeza tafiti, machapisho