Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho ameshtukia mbinu za wapinzani wake katika Michuano ya Ligi ya Mabigwa Barani Afrika Hatua ya Makundi Horoya AC, za kukichunguza kikosichake kabla ya mchezo wa mwishoni mwa juma hili.

Simba SC itakuwa mwenyeji wa Horoya AC katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Jumamosi (Machi 18), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa moja usiku.

Kocha Robertinho amesema anatambua tayari kuna mashushushu wa Horoya wapo jijini Dar es salaam na walifanya kazi ya kukichunguza kikosi chake wakati kikicheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya Jumamosi (Machi 11).

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, ulishuhudia Simba SC ikiifumua Mtibwa Sugar mabao 3-0, huku mshambuliaji Jean Baleke akipiga Hat-Trick ya kwanza akiwa na timu hiyo na kuwa ya sita katika Ligi Kuu msimu huu.

“Tunatambua vizuri wapinzani wetu wapo nchini lakini hilo kwetu halitufanyi kututoa mchezoni kwa sababu bado tuko kwenye ardhi yetu na tunajua ni mchezo wenye umuhimu kwa kiasi gani,” amesema kocha huyo aliyekuwa akiinoa Vipers ya Uganda kabla ya kutua Msimbazi hivi karibuni.

“Kwanza niwapongeze wachezaji wangu kwa ari kubwa waliyoonyesha na kupata matokeo mazuri ambayo yameongeza morali ya timu, hususani katika kipindi hiki ambacho tunaenda kwenye mchezo mgumu, lakini bado tuna kazi kubwa kwenye mechi ya Jumamosi,” amesema Robertinho.

Amesema jambo kubwa linalompa motisha ni kutokana na uwingi wa mabao katika mchezo huo kwa sababu ndio changamoto iliyokuwa inawakabili licha ya kutengeneza nafasi nyingi na wanaenda kukutana na Horoya wakiwa na mzuka mwingi na atawasapraizi uwanjani.

“Kila nafasi ni dhahabu katika hatua hii kwa sababu ni mechi iliyokuwa mikononi mwetu hivyo ni jukumu la washambuliaji wangu kuhakikisha wanaongeza umakini na utulivu kwenye eneo la mwisho hasa kwa michezo iliyosalia ikiwamo miwili ya CAF dhidi ya Horoya na Raja Casabalanca.”

Simba SC inaingia katika maandalizi ya mchezo huo ikihitaji alama tatu tu ili kufikisha tisa zitazoifanya ifuzu moja kwa moja na kuungana na Raja iliyofuzu baada ya kufikisha alama 12.

Mbali na hilo, Simba SC inahitaji kulipa kiasi kutokana na mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Guinea, Februari 11 kuchapwa bao 1-0 licha ya kutengeneza nafasi nyingi na umiliki wa mpira.

Kamala Harris kutembelea Tanzania
Makamu wa Rais ataka ubunifu utatuzi wa migogoro