Wananchi Mjini Njombe wameiomba Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kudhibiti vitendo vya mauaji ya watoto wenye umri kati ya miaka 4-9 ambavyo vinatajwa kuongezeka tangu mwezi disemba mwaka jana na kuendelea kutishia hali ya usalama mjini humo.

Wananchi hao wametoa rai hiyo baada ya mwili wa mtoto mwingine wa jinsia ya kiume kuokotwa kando ya msitu wa asili wa Nundu ulioko nje kidogo ya mji wa Njombe.

“Ni kweli kuna mtoto mwingine amekutwa amefariki pale msituni, tulipofika pale tulitoa taarifa kwa polisi wa kituo cha Uwemba na walivyokuja ni kweli walishuhudia mwili wa mtoto na wakauchukua na kuupeleka mochwari,”amesema Winfrid Mbangala mwenyekiti wa kijiji cha Nundu

Aidha, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Barnaba Baraka amekiri kuupokea mwili wa mtoto huyo na kueleza kuwa bado unafanyiwa uchunguzi huku jeshi la polisi mkoani humo likieleza kuwa taarifa ya tukio hilo bado haijakamilika.

Hata hivyo, matukio ya watoto kupotea na baadhi ya miili yao kuonekana katika misitu inazidi kushika kasi mjini Njombe ambapo katika kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa wilayani humo, watoto 3 wa familia moja wamepotea tangu January 20 mwaka huu.

Kangi Lugola awakuna Watetezi wa haki za binadamu
KKKT Njombe ruksa kuuza viwanja

Comments

comments