Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe leo amezungumzia taarifa zilizokuwa zimesambazwa na kuaminika kwa baadhi ya watu kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa alitoa fedha ili apewe nafasi ya kugombea Urais kupitia chama hicho.

Mbowe Kikao cha Halmashauri Kuu, Mwanza

Akiongea katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho kinachofanyika jijini Mwanza ambacho kitapelekea kumpata Katibu Mkuu Mpya wa chama hicho, Mbowe amesema kuwa Lowassa hakutoa kiasi chochote cha fedha kupata nafasi hiyo.

Alisema taarifa hizo za uongo zilipelekea hata majirani zake kumkejeli kwa kwa kubadili chakula nyumbani kwake.

“Watoto wangu walikuwa wanakula sana maharage, sasa siku moja wakala nyama, jirani akasema umeona Lowassa kaja Chadema,” alisema Mbowe.

Katika hatua nyingine, Mbowe amekemea vitendo vya rushwa vinavyoanza kuibuka katika chama hicho na kueleza kuwa havitavumiliwa na vitakomeshwa haraka kwani vitapelekea kuua chama hicho.

Mbowe alieleza kuwa kutengeneza umoja wa chama hicho na kukijenga kutoka ngazi za chini ni gharama huku akitahadharisha kuwepo kwa mipasuko katika maeneo mbalimbali yaliyopelekea kupunguza ushindi wake katika maeneo husika.

“Migogoro mingi ndani ya Chadema imepelekea kuanguka kwa chama, hivyo itashugulikiwa kwa haraka,” alisema Mwenyekiti huyo wa Chadema.

Chadema yapata Katibu Mkuu Mpya, mfahamu hapa na sifa zake
Afya: Sehemu Tano za mwili wako ambazo hupaswi kuzigusa kwa mkono