Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilitupilia mbali ombi la kuhamishia kesi yao Mahakama Kuu lililowasilishwa na mawakili wanaowatetea Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na wanasheria wa Serikali pamoja na mawakili wa upande wa wawatezi.

Mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Faraja Nchimbi aliiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya upande wa utetezi akieleza kuwa hayakuwa na msingi kisheria na kwamba yalikuwa na lengo la kuipotosha Mahakama.

Nchimbi alifafanua kuwa maombi hayo hayana msingi kwani washtakiwa walisikiliza mashtaka dhidi yao, wakayaelewa na ndio sababu walienda mbali zaidi na kuyapinga. Alidai wasingefanya hivyo kama walikuwa na mtazamo kuwa mashtaka hayo sio halali.

“Kama kweli washtakiwa waliona mashtaka haya si halali, hati ya mashtaka ilitolewa mapema, hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zingewasilishwa kabla washtakiwa hawajajibu kuwa wanakana mashtaka,” alisema Nchimbi.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo na kupanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa leo kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo, mwenyekiti huyo wa Chadema anashtakiwa pamoja na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiku, Katibu Mkuu wake, Vincent Mashinji na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Vigogo hao wa Chadema wanashtakiwa kwa kufanya mkusanyiko usio wa halali na kufanya maandamano yasiyo na kibali yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

 

Video: JPM atoa maagizo 5 mazito mafuta ya kula, Wachungaji wanusurika kichapo baada ya kushindwa kumfufua mfu
Israel, Palestina washambuliana kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa

Comments

comments