Bodi ya Ligi Tanzania bara imetangaza kushuka kwa mapato yanayokusanywa kutokana na viingilio vya watazamaji Uwanjani kwa msimu wa 2019/20 ambapo kilipatikana kiasi cha Bilioni 2.8 ikiwa ndicho kiwango cha chini zaidi tangu msimu wa 2013/14 .

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika semina iliyofanyika katika ukumbi uliopo ndani uwanja wa Benjamin Mkapa, Afisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo Almas Kasongo amesema kwa msimu ulipita watazamaji takribani 480,022 wakati kwa msimu wa 2013/14 idadi ya watazamaji ilikuwa 725,780 ambapo mapato ya viingilio ilikuwa ni Shilingi Billion 3.9.

Kutokana na anguko hilo la watazamaji viwanjani, bodi ya ligi imeandaa jopo maalum la wataalamu watakaofanya tafiti ili kugundua ni kwanini idadi ya watazamaji imepungua uwanjani hususani Jijini Dar es Salaam.

Vilevile TPLB imewaondoa hofu mashabiki wa mpira wa miguu kuwa watatangaza mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu ujao wiki chache zijazo ambapo atachukua nafasi ya Vodacom ambao walijiondoa msimu uliopita.

Katika semina hiyo na Wanahabari za michezo iliyoandaliwa na TFF na bodi ya ligi imetoa elimu juu ya dhumuni la kuwajengea uwezo Wanahabari kuripoti vema habari za michezo zenye lengo la kuinua maendeleo ya soka nchini.

Jerry Muro: Niko bize najenga nchi
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 5, 2021