Wakati tetesi za usajili zikieleza huenda mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba wakamsajili mshambuliaji wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini Justin Shonga, kiungo mshambuliaji wa Young Africans Bernard Morrison amejinasibu kuvuruga dili hilo.

Kwa muda wa majuma kadhaa Shonga amekua akihusishwa na taarifa za kunyatiwa na Simba SC, ambao wamedhamiria kukiboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.

Morisson ambaye aliwahi kucheza mshambuliaji huyo kutoka nchini Zambia katika kikosi cha Orlando Pirates, amesema anaweza kuchukua jukumu la kumshawishi Shonga kujiunga na Young Africans endapo viongozi watamuhakikishia uwezekano wa kumsajili.

“Kweli nimekuwa nikisikia tetesi nyingi sana hapa Tanzania, hasa Simba wakihusishwa kumtaka Shonga na kwamba kuna muda niliona sehemu kama Shonga na timu yake wapo tayari kumuachia kwa dau la milioni 800, jambo ambalo mimi nadhani ni mchezaji anastahili kwenye ligi hii.”

“Nipo tayari kwa timu yoyote kuwasaidia kuzungumza naye, maana ni muda mrefu sasa naona kama hana nafasi sana kwenye kikosi cha kwanza japo uwezo wake ni wa hali ya juu sana.”

“Kama Yanga wakimuhitaji na kuniambia wapo tayari kumpatia dau atakalohitaji mimi sina kipingamizi cha kuwasaidia kwani akija hata kwangu ni msaada mkubwa.” alisema Morrison.

Katika hatua nyingine Morrison amemsifia Shonga kwa kusema ni mshambuliaji mzuri na kama atabahatika kucheza naye kwa mara nyingine tena kama walivyokua Orlando Pirates atafurahia hatua hiyo.

“Shonga ni mshambuliaji mzuri, anajua kufunga na kutumia nafasi anazopata, kama nitabahatika kucheza naye litakua jambo zuri sana kwa sababu mashabiki watafurahi kila siku.”

Morrison ni moja ya wachezaji waliosajiliwa na Young Africans wakati wa dirisha dogo la usajili, na amekua kivutio kikubwa kwa wadau wa soka kutokana na uwezo wake wa kusukuma soka na kuiwezesha klabu hiyo kupata matokeo.

Mwanafunzi miaka 9 abadilika rangi kwa maradhi ya moyo, aomba msaada
Wilshere na stori ya muwa uliozamisha Meli