Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa anatarajiwa kurusha makombora yake ya mwisho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu dhidi mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anayeungwa mkono na Ukawa.

Taarifa za uhakika zimeeleza kuwa Dk. Slaa ambaye ameonekana kuwa nchini wiki iliyopita baada ya kukaa ughaibuni kwa muda tangu alipomvaa Lowassa na Chadema, atapanda katika jukwaa la ACT-Wazalendo kwa lengo la kuyasema yake ya moyoni.

Watu wa karibu wa Dk. Slaa wamelieleza gazeti moja kubwa nchini kuwa mwanasiasa huyo mkongwe amekubaliana na uongozi wa ACT – Wazalendo na atapanda kwa mara ya kwanza katika jukwaa la kampeni la chama hicho, Jumatano (Oktoba 7) akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho katika jimbo la Iringa Mjini, Chiku Abwao.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Dk. Slaa ataendelea na kampeni yake huku akitarajiwa kuilipua Chadema na Ukawa kwa ujumla kwa tuhuma nyingine zinazohisiwa kuwa za kupokea fedha kutoka kwa baadhi ya makada wa CCM ili kuwakubalia kujiunga na chama hicho.

Hivyo, Dk. Slaa atajiunga na Zitto Kabwe ambaye alikuwa naibu Katibu Mkuu wake wakati wakiwa Chadema na kutofautiana kisha chama hicho kumfukuza uanachama chini ya uratibu wa Dk. Slaa. Zitto atampokea Dk. Slaa katika chama chake ACT-Wazalendo ambacho ndiye kiongozi wake mkuu.

Chadema

Awali, Dk. Slaa ambaye alitarajiwa kuwa mgombea urais kupitia Chadema, alifanya mkutano na waandishi wa habari ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha runinga nchini, alionesha msimamo wake wa kupinga kumpokea Edward Lowassa katika chama chache hicho cha zamani. Alimtuhumu Lowassa kwa ufisadi na wizi huku akidai kuwa hana sifa za kuwa kiongozi wa Tanzania.

Aidha, Dk. Slaa alieleza kuwa anapokea vitisho vingi hivyo analindwa na Usalama wa Taifa.

Hata hivyo, Dk. Slaa alikiri katika mahojiano aliyofanya na Star TV kabla hajaenda Ughaibuni kuwa yeye ndiye aliyelipeleka Chadema wazo la kumpokea Lowassa alilolipokea kutoka kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephati Gwajima.

 

 

Lowassa Ampa Mkono Kingunge, Atangaza Neema Kwa Wenyeviti Serikali Za Mtaa
Tanzia: Kama Sio Ajali Ya Gari, Ndoto Hizi Za Mtikila Huenda Zingetimia