Mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya Sekondari Nkomolo, Nkasi mkoani Rukwa, Fredy Pupa (19) ameuawa kwa kuchomwa kisu wakati akicheza kamari baada ya kudhulumiana fedha na mwenzake.

Mkuu wa wilaya ya Nkasi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 29 majira ya saa 11 jioni wakati mwanafunzi huyo akiwa na kijana mwenzake, Samwel Nkoswe (20) wakicheza kamari.

Amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo, alikuwa ameacha shule na alikuwa anaishi mtaani huku akijihusisha na vitendo vya kinyume na sheria kikiwepo cha kucheza kamari.

Imeelezwa kuwa wakiwa wanacheza mchezo huo, mtuhumiwa alikula hela za marehemu lakini alikataa kumpa pesa hizo na kuamua kutoa kisu alichokuwa nacho mfukoni na kumchoma Pupa ubavuni karibu na tumboni.

Baada ya kujeruhiwa mwanafunzi huyo alivuja damu nyingi kitendo kilichompelekea kupoteza maisha muda mfupi baadaye.

Baada ya kuona amefanya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na kwenda kujificha kwenye mashamba yaliyopo kijijini hapo lakini wananchi walimsaka mpaka kumkamata na kisha kuanza kumshambulia, hadi sasa yupo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Justine Masejo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa nduguzake kwaajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi hospitali.

Kila siku watoto wanaungua moto Kahama
Makonda na mkewe wazuiwa kuingia Marekani