Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wake kuwa na mikakati madhubuti kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na itacheza bila Mashabiki kufuatia marufuku iliyotangazwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF kwa kuhofia maambukizi ya Uviko 19 (Covid 19).

Kikosi cha Young Africans kimekamilisha maandalizi ya kuelekea kwenye mchezo huo, ambao unatazamwa kama sehemu ya kujitengenezea nafasi kwa klabu hiyo, kuelekea mchezo wa mkondo wa pili, utakaochezwa mwishoni mwa juma lijalo nchini Nigeria.

Kocha Nabi amesema amewaeleza wazi wachzaji wake kuwa, lengo kubwa kwenye mchezo wa kesho Jumapili (Septemba 12) ni kuona wanashinda mchezo huo kwa mabao mengi, licha ya kutowafahamu vizuri wapinzani wao.

“Najua tunaenda kucheza mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa kwa sababu ya namna wapinzani wetu ambavyo wanacheza lakini kwa kiasi fulani tunashukuru tumeweza kuwajua wapinzani wetu.”

“Kikubwa ni kuona kwamba tunashinda kwa mabao mengi kwa sababu hiyo itakuwa ngao yetu hata kwenye mchezo ujao wa marudiano ingawa bado hauwezi kuwa mchezo mwepesi.” amesema Kocha Nabi

Kwenye mchezo wa kesho pia mashabiki wa Yanga watakuwa na fursa ya kuona namna Nabi atakavyoanzisha jeshi lake la kazi kwenye kusaka ushindi katika mchezo huo.

Ni Ditram Nchimbi na Heritier Makambo wanapewa nafasi ya kuongoza safu ya ushambuliaji katia mchezo huo huku Fiston Mayele yeye ishu ya vibali vya kazi ikiwa ni kikwazo kwake.

Wengine ni Shaban Djuma huyu ni beki pamoja na Khalid Aucho huyu ni kiungo nao pia wanatatizo la kutokuwa na ITC.

Simba SC yavunja ukimya, ujio wa Hitimana Thiery
Tanzania kufaidika na Royal Tour kimataifa