Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa umeme Kinyerezi II na ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha mradi huo unazalisha megawati 30 za umeme nchini ifikapo Desemba mwaka huu

Kalemani amefanya ziara hiyo ya kushtukiza mapema leo Juni 30, 2017 ili kujua hali ya utendaji ambapo amesema taarifa aliyopewa tangu alipowasili ni kuwa mradi huo utazalisha megawati 240 utakapokamilika mwakani ila 30 zikamilike Desemba mwaka huu.

“Mradi wa Kinyerezi II tunategemea utupatie megawati 240, lakini lazima tuanze kupata hizo mapema, kwa taarifa niliyosikia tutaanza na megawati 30 sasa niseme megawati hizo tupate ifikikapo Desemba,” amesema Kalemani.

Kalemani amesisitiza kuwa zitakazobakia apewe ratiba za utekelezaji wake ili hadi kufikia Septemba 2017 megawati zote ziwe tayari.

Amesema kuwa hakutakuwa na uongezaji wa muda katika miradi yote miwili ya Kinyerezi I na II hivyo kuwataka wahusika kufanya kazi kwa nguvu na weledi ili kumaliza kazi, pia amesema mradi wa Kinyerezi I umefikia asilimia 35 hali ambayo hairidhishi huku ukitegemewa kutoa megawati 185 kufikia Agosti 2017.

“Kufikia Septemba mwakani, tunategemea kuwa na megawati 425 kwa miradi yote miwili bila kupungua, fanyeni kazi sana katika Kinyerezi I,” amesema Kalemani.

Naye Mkurugenzi wa Tanesco, Tito Mwinuka ameomba ushirikiano baina ya Serikali na Shirika hilo ili kufika malengo ya agizo la Naibu Waziri.

“Tushirikiane pamoja Tanesco na Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kwamba mradi ukamilike kwa wakati,” amesema Mwinuka.

 

Ivan Gazidis Awapigia Magoti Mashabiki
CCM yamng’ang’ania Lowassa, mwenyewe akomaa na yake