Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameendelea kusisitiza msimamo wake kuhusu mabadiliko ya kifungu cha sheria ya Zao la Korosho, akiwataka wananchi wake waamini kuwa ataendelea kuwatetea kwani ameyatoa maisha yake kwa ajili yao.

Akihutubia jana kwenye mkutano wa hadhara jimboni kwake, Nape amesema kuwa mabadiliko yaliyofanyika kwenye sheria hiyo ambayo hivi sasa yanaipa mamlaka Serikali kuchukua ushuru wote unaotokana na kuuza korosho nje ya nchi, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Serikali ilichukua asilimia 35 na Mfuko wa Pembejeo asilimia 65, yasipoleta matokeo chanya Serikali iwaombe radhi wananchi au ikiwa na matokeo chanya yeye ataomba radhi.

Nape ambaye aliungana na wabunge wengine 16 wa Kusini kupinga vikali bungeni mabadiliko hayo, alidai kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuua kilimo cha korosho kwa wananchi wanyonge na kwamba ilikuwa kinyume na ahadi ya CCM kwa wananchi hao.

Ingawa mabadiliko hayo yalipitishwa baada ya kupigiwa kura na wabunge wengi kwa mujibu wa taratibu za kibunge, Nape amesisitiza kuwa amesema ukweli kama chama chake kinavyosimamia.

“Mmi nimetoa maisha yangu. Potelea mbali. Lakini kusema ukweli tutasema na chama changu kinasema ‘nitasema ukweli daima, fitna kwangu mwiko’,” alisema Nape.

“Nyekundu iwe nyekundu, kama wakubwa watachukia, watachukia. Nyekundu iwe nyekundu na nyeusi iwe nyeusi,”aliongeza.

Mwanasiasa huyo ambaye pia alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alidai kuwa mapendekezo ya mabadiliko ya kifungu husika yalianza baada ya ushuru unaotokana na kuuza korosho nje kupanda kutoka Sh800 milioni hadi Sh200 bilioni.

“Tumepigania hela yetu tumeambiwa sio yetu, Alhamdullilah, tunamshukuru Mwenyezi Mungu. Twende halafu huko mbele tutaona nani alikuwa mkweli,” Nape anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Nape aliwataka wananchi wake kutokuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wake ndani ya chama akidai kuwa ana hisa nyingi ndani ya chama hicho hivyo wasiwe na wasiwasi.

“Yapo maneno sasa, hatima ya mbunge wetu ni ipi? Tusipate shida. Kwenye chama changu cha kijani nina hisa nyingi msipate shida. Najua mmenielewa. Furaha yangu ni kuwatumikia ninyi,”alisema.

Nape alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na sasa amebaki kuwa Mbunge akileta changamoto kadhaa kwenye mijadala ya Bunge na kuhamasisha majadiliano.

Son Heung-min azuiwa Korea Kusini
Wastaafu kabla ya 1999 kuanza kulipwa

Comments

comments