Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye amesema kuwa yapo mambo ambayo amekuwa akijifunza kutoka kwa aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kutokana na uzoefu wake katika siasa.

Nape alitoa kauli hiyo wiki iliyopita alipofanya mahojiano maalum na gazeti la Jambo Leo mjini Dodoma ambapo mikutano ya Bunge la Kumi na Moja inaendelea.

Alisema kuwa ingawa amekuwa akipinga baadhi ya mambo ya Lowassa, ni mwanasiasa anayemheshimu na kwamba kutokana na umri wake katika masuala ya siasa yapo mambo mengi ambayo amekuwa akijifunza kutoka kwake.

Katika hatua nyingine, Nape alisema kuwa uamuzi wa Lowassa kukubali matokeo japo kwa shingo upande, kulisaidia katika kuiweka nchi katika hali ya amani baada ya uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkubwa kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

“Na uamuzi wake huo unaimarisha sana demokrasia katika nchi yetu. Ukishinda ni vizuri kumshukuru aliyekubali kushindana na wewe,” Nape anakaririwa na gazeti hilo.

Alisema kuwa hajawahi kukutana na mwanasiasa huyo mkongwe tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu lakini atakapokutana naye atampa pole kwa matokeo ya uchaguzi na anaamini yeye pia atampongeza kwa kushinda uchaguzi kwakuwa katika siasa huwa hakuna hasira.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM ambaye hivi sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa akimpinga hadharani Lowassa katika hatua yake ya kutaka kugombea urais kupitia chama hicho na kuegeuka kuwa hasimu wake mkuu tangu akiwa ndani ya chama na hata alipohamia Chadema.

Asimulia Maisha ya Kitwanga baada ya kutumbuliwa
Audio: Utazidisha heshima kwa Ngwair ukisiliza alichowasilisha hapa DJ K-U