Sifahamu kama kabila langu (Wapogoro) kama wana utani na Wakwere, lakini Wakwere walikula mkojo. Kumbuka neno CHIJAMAKOZO inatokana na maneno mawili ya Kikwere CHIJA+MAKOZO, maana ya CHIJA ni KULA, MAKOZO ni MKOJO kwa hiyo CHIJA MAKOZO ni KULA MKOJO.

Hayo yalikuwa maneno yangu ya mwisho katika makala yangu iliyopachikwa jina ya NJAA YA CHIJAMAKOZO ambapo inaaminika kuwa wakwere walichemsha virago vyao vya ngozi za wanyama walizokuwa wakilalia na kula kuepuka kufa kwa njaa.

Mara baada ya matini hiyo, nilipigiwa simu na Wakwere wengi kwanza wakishukuru kwa kuwatania, lakini mimi niliwaambia sikuwa nawatania bali nilikuwa nawaeleza ukweli, kwa hoja ya kutokufahamu ukweli wa utani baina ya Mpogoro na Mkwere.

“Wakwere na Wapogoro wana utani mkubwa na mkubwa zaidi hata zaidi ya Wasukuma na Wanyamwezi.”

Ndugu yangu huyo aliyeanza kunijulisha hilo alikuwa ni Mkwere wa Dar es Salaam, tuliyesoma wote huko Tambaza Sekondari. Ndugu yangu huyu Baba yake ni Mkwere lakini mama yake Myao. Yeye kaoa (mke) Mhindi (Goa) lakini mama yake Myao.

Nilimtania ndugu yangu huyu juu ya kabila la Watoto wake kwani UKWERE+UYAO (BABA),GOA+UYAO(MAMA) nilisema kuwa watoto wake ni Wayao akaniambia hapana ni Wakwere. Akidai kuwa wao wanachukua ukoo kwa baba. Niliendelea kumnanga kuwa sasa Ukwere wenyewe una nafasi ndogo sana, ndugu huyu alicheka mno.

Ndugu huyu ambaye alikuja Dar es Salaam kusoma nilimwambia kuwa Wakwere wengi waliosoma enzi hizo lazima walipitia Tambaza Sekondari, kwao hawakuwa na shule nzuri hadi kusoma Dar es Salaam ili kufuta ujinga? Nilimuuliza kwa utani na alicheka tuu.
Ndugu huyu aliniunganisha na ndugu Augustino Meli ambaye ni Mkwere wa Lugoba anayeufahamu kidogo utamaduni na maisha ya Wakwere.

“Ndugu Meli aliniambia kuwa Wakwere, Waluguru, Wabena Manga, Wabena na Wapogoro wote hao wanatokea Kusini na walipokuwa wakisafiri wakawa wakibadilika kulingana na mazingira mbalimbali waliyokutana nayo.”

Wapogoro nao walikuwemo katika msafara huo wakashuka Ifakara na kuelekea huko bondeni hadi Mahenge na hata wakashuka zaidi, huko walikuwa wakikutana na eneo ambalo Wagoni walifika kuwinda linalofahamika kama Lukumburu.

Mara baada ya safari hiyo pale Mpogoro alipotembelea maeneo ya Wakwere/Wakwere kwenda eneo la Wapogoro kukumbuka vituko vya safarini njiani walivyokuwa wakiishi na hapo ndipo utani ukaja

Ndugu Meli aliniambia kuwa ukifika Madaba unakutana na koo kama akina Kibena, Mwenda, hata walipofika Morogoro akina Mwenda. Hata akina Kingaru wa Kinolei ni Wabena na Wakwere wana akina Mlambena, Mbena akina Manguo yote hiyo ni kuonesha kuwa hawa ni ndugu.

Waluguru na Wakwere ni mtu na mjomba wake lakini Wakwere na Wapogoro ni watani tena watani ndugu kuliko makabila mengine.

“Panapotokea msiba wa Mkwere, Wapogoro wanaweza kusema kuwa hapa mzigo (Jeneza) hauondoki mpaka kutolewa kitu kidogo, kweli jeneza haliwezi kuinulia hadi mtani apatiwe chake. Hapo ndipo maziko yatafanyika.

Hivyo ndivyo Wapogoro na Wakwere wakawa watani hadi sasa. Nikutakie siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Mukoko amerudi Young Africans
Waziri Ummy aja na kasi mpya