Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanajipenyeza kupitia mgongo wa taasisi za dini nchini kujifanya wahubiri kumbe ni wachochezi na wanajiingiza katika masuala ya kisiasa.

Amesema kuwa wizara yake ipo makini katika kusajili Makanisa na Misikiti yote nchini na mpaka sasa wana maombi mengi ambayo yametumwa wakiomba kusajiliwa ambapo baadhi yao bado hayajasajiliwa kwasababu wanahitaji umakini mkubwa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sunsi, Kata ya Nampindi, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, ambapo amesema kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa nchini na uwepo wao ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

“Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ya Awamu ya Tano haitakua tayari kwa mwananchi yeyote kutumia mwavuli wa dini, au kufanya misikiti na makanisa kuwa kichaka kwa kufanya uchochezi katika nchi hii, kuhatarisha amani ya nchi hii, tupo makini na hatuwezi kuchezewa na mtu yeyote au taasisi yoyote,” amesema Lugola.

Hata hivyo, Lugola ameongeza kuwa Serikali haitakubali kuchezewa na kutokana na sababu hizo na nyinginezo Wizara yake inaendelea kuwa makini kuyafanyia kazi maombi ya taasisi hizo kwa kuomba usajili, na aliwataka ambao wametuma maombi yao kwa muda mrefu waendelee kusubiri wakati Serikali ikiendelea kuwa makini kuyafanyia kazi maombi yao.

 

Afrika yaongoza kwa rasilimali ya maji baridi
Marekani wamepanga kuniua'Hawaniwezi'- Nicolas Maduro

Comments

comments