Usiku wa kuamkia leo, Tyson Fury amethibitisha kuwa ndiye bondia mbabe zaidi wa uzito wa juu kwa sasa baada ya kumpiga mpinzani wake Deontay Wilder katika pambano lao la tatu kuwania Mkanda wa Ubingwa wa Dunia Uzito wa Juu (WBC heavy weight tittle).

Pambano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa T-Mobile Arena, Nevada nchini Marekani lilikuwa kali na zito kuliko mapambano yao mawili ya awali, Wilder alifanikiwa kumuangusha Fury mara mbili katika raundi ya nne, naye akaangushwa mara kadhaa.

Hata hivyo, Fury alifanikiwa kumaliza pambano katika raundi ya 11 akimpiga chini Wilder ambaye alionekana akiwa amechoka lakini bado akiwa ni hatari kwa mashambulizi ya kushtukiza.

Pambano hilo limetajwa kuwa kati ya mapambano bora zaidi kuwahi kutokea katika muongo huu, kwenye kilinge cha uzito wa juu.

Promota mkongwe, Bob Arum amesema kuwa hili lilikuwa pambano bora zaidi ambalo amewahi kushuhudia kwenye maisha yake.

“Nimekuwa kwenye hii biashara ya ngumi kama promota kwa miaka 57, kwakweli sijawahi kushuhudia pambano la uzito wa juu la kipekee na lenye mvuto kama hili,” alisema Bob Arum.

Alisema kuwa ingawa Wilder amepoteza pambano hilo, ameonesha kuwa ana moyo wa mpambanaji wa kweli.

Pambano lao la kwanza walimaliza kwa suluhu/sare, pambano la pili Fury alishinda kwa KO lakini kulikuwa na malalamiko kuwa alifanya udanganyifu katika gloves alizotumia. Pambano hili la tatu limemaliza ubishi kati yao.

Fury anabaki kuwa ndiye bondia wa uzito wa juu ambaye hajawahi kupoteza pambano, wakati Wilder aliyekuwa na rekodi hiyo akipoteza mapambano mawili yote mikononi mwa Fury.

Uzinduzi wa kampeni ya maendeleo na mapambano dhidi ya Uviko 19
Vijana waongoza matatizo ya akili, vilevi vikitajwa kuwa ni sababu