Kivuli cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuwagharimu baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa majina yao kukatwa katika uchaguzi wa wenyeviti wa wilaya.

Viongozi hao walipitiwa na panga hilo baada ya kubainika kuwa na hatia katika kigezo cha kuwang’oa watu wanaoonekana kuwa na hali ya kumuunga mkono Lowassa hivyo kuwa na sifa ya usaliti ndani ya chama hicho.

Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana hivi karibuni Ikulu jijini Dar es Salaam iliyaondoa majina ya viongozi hao kwa kutumia vigezo kadhaa, vikuu vikiwa ni suala la usaliti na kuwa na vyeo zaidi ya kimoja ndani ya chama au kuwa watumishi Serikalini. Gazeti la Mwananchi linavikariri vyanzo vyake.

Panga hilo limepita ndani ya jiji la Dar es Salaam na kuwaondoa ‘wasaliti’ kwenye orodha ya wagombea ikiwa ni pamoja na wakuu wa wilaya ya Ilala na Kinondoni.

Katika mkoa wa Iringa, wenyeviti wake wote wameondolewa kwenye orodha ya wagombea. Mji huo ulitajwa kuwa moja ya eneo ambalo lilikuwa na mgogoro mkubwa kuhusu sakata la wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Katika mkoa wa Mara, wenyeviti wa wilaya ya Bunda (Chacha Gimwana) na wilaya ya Tarime (Rashidi Bugomba) waliondolewa, maeneo ambayo CCM pia ilipoteza viti vya ubunge.

Mikoa 33 ya Tanzania Bara na Visiwani imekumbwa na mtikisiko wa ‘panga pangua’ ya wagombea wa nafasi hizo ndani ya CCM.

Nassari asubiri ushahidi mwingine kutoka Arusha
Rais apewa ‘onyo la mwisho’