Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana aliyetoa salamu ya ‘Kidumu Chama Cha Mapinduzi’ akiwa amevalia sare za jeshi hilo ameweka mkazo kwenye kauli yake.

Kamanda Shana alitoa salamu hiyo wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere wilayani Butiama, Oktoba 13 mwaka huu, ambapo alisema ili kumuenzi mwalimu ni lazima Chama Cha Mapinduzi kiendelee kudumu milele.

“Leo naomba niwafundishe salamu mpya, nikisema kidumu Chama Cha Mapinduzi mnatakiwa kuitikia ‘kidumu milele’,” alisema Kamanda Shana na kuendesha zoezi hilo kwa mafanikio.

Akihojiwa kuhusu kauli hiyo iliyozua mijadala kwenye mitandao ya kijamii hasa kuhusu maadili ya jeshi hilo, alisisitiza kuwa hakuna kosa alilofanya na anasimamia alichokisema.

“Nasema hivi, ile haikuwa sherehe ya CCM, yalikuwa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 19 tangu kufariki Baba wa Taifa. Nikawaambia njia pekee ya kumuenzi baba wa taifa ni kutaka chama alichokiasisi kidumu, ambacho ni CCM,” Mwananchi inamkariri Kamanda Mshana.

“Hata leo ukiniuliza unamzungumziaje Mwalimu Nyerere, nitajibu kidumu Chama Cha Mapinduzi ambacho alikiasisi,” aliongeza.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alieleza kutokubaliana na alichokifanya Kamanda Mshana akieleza kuwa anachofahamu ni kwamba Jeshi hilo halifungamani na chama chochote cha siasa.

Kamanda Ndaki alihoji kuwa kwa kufanya hivyo, vyama vingine vya siasa vitalielewaje jeshi hilo.

Mwanafunzi aua wenzake 19 kwa risasi, ajiua
HELSB yawafungulia milango wanafunzi

Comments

comments